32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema watangaza wiki ya maandamano

Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Benson Kigaila
Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Benson Kigaila

NA SHABANI MATUTU Dar

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuanza kutekeleza maadhimio ya Mkutano wake Mkuu, kuanzia leo hadi Jumamosi kwa kufanya maandamano na migomo isiyo na ukomo nchini kote.

Akitangaza utekelezaji wa maazimio hayo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Benson Kigaila, alisema kuwa chama hicho lazima kitekeleze maazimio ya Mkutano Mkuu.

“Maandamano yaliyokuwa siku chache zilizopita yalikuwa rasharasha sasa mvua ya mawe inaanza  hadi jumamosi, na ninawahakikishia hakuna rangi wataacha ona,” alisema.

Kigaila alisema maandamano hayo yatafanyika kwa awamu ambako leo yataanza na mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa huku kwa Mkoa wa Dar es Salaam yanatarajiwa kufanyika Jumatano.

Alisema kuwa, maandamano hayo yataratibiwa na uongozi wa wilaya ya chama hicho na kuishia kwa Mkuu wa Milaya na kwamba kwenye ngazi ya Mkoa hali itakuwa hiyohiyo.

Akielezea sababu ya kufanya maandamano juma hilo aliloliita, ‘wiki ya maandamano na migomo’ alisema lengo ni kulazimisha usitishwaji wa Bunge Maalum la Katiba ili kuokoa fedha za walipakodi.

Kuhusu uhalali wa chama hicho kutaka kulazimisha usitishwaji wa Bunge hilo, alisema wamefanya hivyo ili kulinda Katiba ya Nchi.

“Katiba Ibara 27 (1) inasema kila raia wa Tanzania anayohaki na wajibu wa kulinda mali ya nchi na rasilimali ya nchi ili itumike sawasawa kwa manufaa ya Watanzania.

Hivyo kwa kutumia kifungu hicho Chadema inaowajibu wa kulinda rasilimali za nchi kwa sababu Katiba inatulazimisha kufanya hivyo,” alisema Kigaila.

Kuhusu uhalali wa maandamano hayo, Kigaila alikiri na kusema kisheria ni halali kwa kutumia Ibara ya 20 ya Katiba inasema kuwa kila mtu anayohaki ya kuandamana.

“Ukitazama katika sheria za vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 (11) aya ya kwanza inasema kwamba ukitaka kufanya maandamano au mkutano unachotakiwa ni kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ndani ya saa 48, na ukishatoa unatakiwa kuendelea na maandalizi ya shughuli yake na si kuzuiliwa,

“Nimesikitishwa na baadhi ya wakuu wa polisi katika wilaya nyingine kwa kuwagomea viongozi wetu, kuandamana kwa sababu dhaifu wakieleza kwamba eti Bunge linaloendelea lipo kisheria. Maandamano yapo palepale kwa sababu zuio waliyotoa haikidhi vigezo vya kisheria,” alisema.

Kigaila alitoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu kutoa ulinzi kwa maandamano hayo ya amani, huku akitoa tahadhari kwamba kama hawatakuwa na askari wa kutosha awaeleze ili watumie vijana wao wa chama kulinda maandamano hayo ambayo amesema yatatumia mbinu 148.

“Tutahakikisha tunazuia wizi wa fedha za wananchi unaoendelea Dodoma huku wakijua fika hakuna Katiba itakayopatikana baada ya kumalizika kwa Bunge,” alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walikutana na Rais Jakaya Kikwete mara mbili ili kutafuta muafaka wa Katiba na wote kwa pamoja walikubaliana kwamba ilikuwa vigumu kupatikana kwa Katiba bora itakayofaa.

Alibainisha kuwa, baada ya kukaa na kamati ya ufundi ya Ukawa wameamua kushirikiana na vyama vinavyounda umoja huo katika kushiriki kikamilifu.

Alisema kuwa kwa upande wa maandamano ya Dodoma yataelekea kwenye Bungeni na kwa Dar es Salaam wakisiposikilizwa watapeleka malalamiko yao kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Lipumba aunga mkono

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba ameunga mkono maandamano yaliyoratibiwa na Chadema ili kupinga kuendelea kwa Bunge la Katiba.

Akizungumza na waandishi bwa habari jijini Dar es Salaam jana alisema kuwa wanaunga mkono maandamano hayo kwa sababu yanalenga kupigania haki za watanzania.

Alisema Rasimu Mpya ya Katiba katika kifungu cha 31 kinaainisha vizuri kuwa kila mtu anayo haki ya kupata, kutoa na kutafuta habari bila ya kubugudhiwa na mtu yeyote.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles