Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amefichua kuwa anakusudia kusomea ukocha baada ya kustaafu soka.
Akizungumza na MTANZANIA, Cannavaro alisema anataka kusomea taaluma hiyo ili aje kuchukua mikoba ya kocha wake wa sasa wa timu hiyo, George Lwandamina.
Cannavaro ambaye tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu hajaichezea Yanga mchezo hata mmoja, amekuwa akijifunza vitu vingi kutoka kwa kocha wake huyo ambavyo anaamini vitamsaidia pale atakapoamua kufanya kazi ya kufundisha.
“Hakuna kinachoshindikana kwani katika kipindi cha misimu 11 nilichoichezea Yanga nimejifunza mambo mengi.
“Kwa kuwa lengo langu ni kusomea ukocha baada ya kustaafu naamini yatanisaidia sana katika kuifanya kazi kwa ufanisi,” alisema.
Cannavaro alijiunga na Yanga mwaka 1997 akitokea timu ya Tembo ya Zanzibar.