MSIMAMO wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wa kukataa kuwajibika baada ya kuhusishwa na kashfa ya ukwapuaji wa Sh bilioni 300 zilizokuwa zimehifadhiwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, sasa umeanza kutafasiriwa kuwa ni ung’ang’anizi wa madaraka.
Tafasiri hii imeanza kutolewa sasa ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu Bunge la Jamhuri lilipopitisha maazimio nane yanayotakiwa kufanyiwa kazi na Serikali baada ya kutolewa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya Escrow, likiwemo la mamlaka ya uteuzi ya Waziri Muhongo kumuwajibisha sambamba na watendaji na viongozi wa kisiasa walioguswa na sakata hilo.
Hadi sasa azimio hilo halijatekelezwa na mamlaka zilizomteua na mwenyewe Waziri Muhongo ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutoachia ngazi kwa kile alichokieleza tangu kuibuliwa kwa kashfa hiyo kuwa fedha zilizokwapuliwa siyo za umma, msimamo ambao unatofautiana na ripoti za uchunguzi za vyombo vya dola na Bunge.
Katikati ya sintofahamu hii, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ambaye alianzisha uchunguzi wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ametoa kauli ya kuwashangaa viongozi wa Serikali wanaong’ang’ania madaraka hata baada ya kukataliwa na wananchi.
Utouh alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika mdahalo uliofanyika wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Mwanzilishi na Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Twaweza, Rakesh Rajan, anayekwenda kufanya kazi katika Taasisi ya Kimataifa ya Ford, yenye makao yake jijini New York, Marekani ambayo inajishughulisha na mambo ya demokrasia, uwajibikaji na shughuli za Serikali.
Akichangia mada ya namna bora ya kupunguza upotevu wa rasilimali za taifa ambayo iliibua mjadala mkali miongoni mwa wajumbe, Utouh alisema viongozi kutokuwa wawazi na wawajibikaji kwa jamii ndiyo msingi wa mmomonyoko wa maadili ambao umekuwa na athari mbaya kwa jamii nzima.
Katika mjadala huo uliokuwa ukiongozwa na mwanahabari mkongwe ambaye ni mwanasheria kitaaluma, Jenerali Twaha Ulimwengu, Utouh alisema viongozi wa Serikali wanaotuhumiwa kwa makosa yaliyofanyika kwenye ofisi wanazozisimamia, wanapaswa kujenga utamaduni wa kuwajibika badala ya kung’ang’ania madaraka.
Ingawa Utouh hakutaja jina la kiongozi yeyote wa Serikali aliyeng’ang’ania ofisini licha ya Bunge na makundi mbalimbali ya jamii kumtaka aachie ngazi kutokana na jina lake kutajwa kwenye kashfa, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo, ndiye aliye katika shinikizo hilo kwa sasa.
“Kama watu unaowaongoza wanapinga uwepo wako na kukutaka kuwajibika kwanini unaendelea kung’ang’ania? Pia kwanini Serikali inaendelea kulipa fedha kwa wafu. Wewe ni kiongozi na watu hawaridhiki na wewe kwanini usubiri wakufukuze? Inatakiwa utoke mwenyewe.
“Katika uwajibikaji ningependa kuona viongozi wanawajibika, hata hivyo kama unaowaongoza wana mashaka na wewe hata kama ukiwa mtendaji mzuri ni lazima uwajibike si kung’ang’ania uongozi,” alisema Utouh.
Alisema ripoti ya CAG iliyochunguza kashfa ya Escrow haijafanyiwa kazi ipasavyo na Serikali licha ya kuwagusa baadhi ya watendaji na viongozi wa Serikali ambao wanapaswa kuwajibika ili kujenga utamaduni wa viongozi kuiishi misingi ya utawala bora.
Kauli hiyo ya Utouh ilishabihiana kwa kiwango kikubwa na iliyotolewa na Jaji Joseph Sinde Warioba, ambaye pia alipata nafasi ya kuzungumza katika mjadala huo na kueleza kuwa ni muhimu viongozi wa Serikali kuzingatia uwajibikaji na Bunge kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wa Serikali kuu wanaopinga kuwajibika wenyewe.
Jaji Warioba alisema Tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wake, iliweka kifungu kinacholipa Bunge nguvu ya kuwawajibisha viongozi wa Serikali lakini Bunge la Katiba likakitoa.
Alisema hata Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imefanya mambo mbalimbali ikiwemo kutaka mikataba ya gesi kuwekwa wazi lakini Serikali haitaki kuionyesha.
“Zitto (Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe) angekuwa hapa angeweza kulieleza vizuri hili suala, bila kuhakikisha uwepo wa uwajibikaji na uwazi hakuna kitachofanyika katika maendeleo,” alisema Warioba.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi katika mahojiano maalumu nje ya ukumbi wa Karimjee mahali ulipokuwa ukifanyika mdahalo huo, Zitto alisema uwajibikaji utawafanya watu wenye mamlaka kutekeleza wajibu wao na tatizo kubwa linaloiandama nchi yetu la kutokuwa na mfumo wa kuwajibishana.
“Kutokuwa na mfumo kunasababisha watu kufanya mambo wanavyojisikia iwe kwenye elimu au katika sekta nyingine hakuna uwajibikaji.
“Tanzania siku zote hakuna mfumo wa uwajibikaji, hilo ndilo kosa alilokosea Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere matokeo yake hali ya rushwa imekuwa kubwa, siku hizi hakuna mfumo wala mtu wa kuogopwa,” alisema Zitto.
Novemba mwishoni, 2014, Bunge lilipitisha maazimio nane likiwamo linaloitaka Serikali kuwawajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Maswi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema.