32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Buhari Rais tena wa Nigeria: Miaka minne imepotea bure.

Othman Miraji

MUHAMMADU Buhari wa Nigeria (76) ameukata tena. Kura milioni 15.1 zimetosha kwa yeye kuendelee kwa miaka minne ijayo kuitawala nchi hiyo ya Afrika Magharibi na yenye wakaazi wengi kabisa (milioni 190) katika bara hilo.

Hiyo ina maana ya kupotea bure miaka mingine minne, kwani tangu Buhari aliposhika madaraka Mwaka 2015 hajafanya kubwa la maana kwa nchi yake.

Aliahidi mambo mengi katika kampeni za uchaguzi wa 2015: kuwashinda na kuwatokomeza wanamgambo wa kigaidi wa Boko Haram, kupambana vilivyo na rushwa na kuupiga jeki uchumi wa nchi.

Mtu yeyeote anayeitembelea Nigeria hivi sasa atagundua kwamba Boko Haram bado iko hai na maeneo ya mizozo imeongezeka, licha ya kutaja mapambano yasiyokwisha baina ya wakulima na wafugaji na ambayo yanasababisha vifo vya raia. Kuna pia waasi, watu waliochukua silaha wanataka maeneo yao yanayotoa mafuta yatengewe fedha zaidi kutoka serikali kuu.

Hivi sasa zaidi ya Wanigeria milioni 91 wanaishi katika umaskini hohehahe, kwa wastani kila mmoja akiwa na kipato cha dola 1.90 kwa siku. Mfumuko wa bei za bidhaa- asilimia 11.37 kila mwaka, hauzuiliki na hakuna maelezo yanayoingia akilini kwamba kweli serikali sasa itaweza kuzidhibiti changamoto zilizoko mbele yake. Kinyume. Buhari, ambaye Mei mwaka jana alibakia London zaidi ya miezi mitatu kwa ajili ya matibabu, anaonekana amechoka, ni dhaifu kimwili.

Mshindani wake, Atiku Abubakar, hakuja na mbadala wowote wenye kuwavutia wananchi, hajafafanua muono wake juu ya Nigeria, nchi iliyogawika kisiasa, kiuchumi na kijamii. Amejitambulisha tu kwamba anapendelea siasa za uchumi wa kiliberali.

Naye si umri (72) mdogo, na anatajwa amejipatia utajiri mkubwa na wa haraka kwa njia za wasiwasi. Hata hivyo, kama alivyo Buhari, Abubakar pia ni wa kutoka tabaka la wanasiasa wakongwe ambao wamebadilishana madaraka mnamo miongo ya miaka. Wote wawili ni wa kutokea kaskazini ya nchi hiyo na ni Waislamu.

Angalau sasa mabadiliko huenda yatatokea, japokuwa kidogo, kama ilivyojiri huko Ivory Coast, Mali na Burkina Faso, pale wanasiasa wakongwe waliposafisha njia na si kumfungulia njia mtu yeyote aingie madarakani ilimradi tu awe chini ya ushawishi wao.

Kumeasisiwa huko Nigeria vuguvugu linaloitwa: Wewe si Kijana hivyo. Gombea Uchaguzi, ambalo limefaulu katika kampeni yake kutaka umri wa mtu kuruhusiwa kupiga kura ushushwe nchini humo.

Malalamiko ya jumuiya za kiraia hayatoshi, lazima masuala hayo yapiganiwe pia katika majukwaa ya siasa na hasa watu waungane mkono. Ilivyokuwa kulikuwapo wagombea 73 wa urais mara hii, kwa mara nyingine tena hamna jipya kabisa lililotokea.

Upinzani uliogawika ndio umekuwa uhakikisho ulio bora kabisa kwa vizee kubakia katika madaraka. Vizee hawalazimiki hata kufanya kazi sana ili kubakia katika hatamu za serikali kwa vile vijana, kwa vyovyote, wamegawika- madaraka yako mbali nao, wanayaotea tu.

Tume ya Uchaguzi ya Nigeria ilikifanya kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi kiwe kigumu na pia cha kusisimua. Alfajiri ya Jumatano, siku nne baada ya uchaguzi wa Jumamosi, Tume hiyo ilitangaza kuchaguliwa tena Buhari. Jenerali huyo wa jeshi aliyebadilika sasa kuwa mwanasiasa alipata kura milioni 15.1, kura milioni nne zaidi ya zile za  mshindani wake, Atiku Abubakar.

Siku moja kabla ilionekana wazi kwamba Buhari ndiye mshindi. Tangu Jumanne alasiri ulisambazwa ujumbe kupitia mitandao uliomtaka Abubakar akiri hadharani kwamba ameshindwa.

Lakini tangu Jumatatu chama chake cha People’s Democratic kilitangaza kwamba hakitayatambua matokeo kwa vile kulikuwapo uchakachuaji katika uchaguzi huo. Kwa watu wengi tamko hilo lilichukuliwa ni kukubali mapema kushindwa.

Baada ya kukaa kimya kwa masaa, Atiku alitoa tamko kuhusu matokeo hayo: Pindi ningekuwa nimeshindwa katika uchaguzi huru na wa haki, bila ya kuchelewa ningempongeza mshindi. Ilivyokuwa hilo si lililotokea, basi ninayakataa matokeo na nitashtaki kuyapinga.

Kwa Atiku Abubakar, ambaye alikuwa makamo wa rais wa nchi baina ya 1999-2007, uchaguzi huu ulikuwa muhimu, wa kufa au kupona.

Ndani ya chama chake aliweka mbinyo ateuliwe kuwa mgombea na aliwakusanya wasaidizi wake nchi nzima wamfanyie kampeni. Yawezekana kwamba hii ilikuwa nafasi yake ya mwisho kugombea wadhifa huo wa juu kabisa nchini.

Haitarajiwi kwamba upinzani utachukua sheria mikononi mwake na kufanya fujo kuyabisha matokeo hayo: Nigeria haihitaji tena fujo na matumizi ya nguvu,  alisema Idayat Hassan, Mkuu wa Kituo cha Demokrasia na Maendelo kilichopo katika mji mkuu wa Abuja.

Uchaguzi huo wa urais, ambao ulikwenda sambamba na wa Baraza la Senate na Bunge la nchi nzima, tangu mwanzo ulikumbwa na matatizo. Peke yake katika Mkoa wa Rivers, watu 942,368 hawajaweza kupiga kura. Nchini kote, kutokana na fujo na njia mbaya za usafiri, asilimia 3.3 ya watu walioandikishwa kupiga kura hawajaweza kuitumia nafasi hiyo. Hao ni mara nne zaidi kuliko wale wa mwaka 2015. Lakini kura za watu hao hata zingepigwa zisingebadilisha matokeo.

Makisio ya jumuiya za kiraia zilizokuwa na zaidi ya wachunguzi 8,800 kuufuatiliza uchaguzi huo ni kwamba watu 47 walikufa siku ya uchaguzi kutokana na ghasia na fujo. Kulikuwapo taarifa za watu kutishwa na pia kura kununuliwa.

Cha kushangaza ni kwamba si watu wengi waliojitokeza kupiga kura. Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi waliopiga kura walifikia karibu ya asilimia 36 ya watu walioandikishwa.

Hiyo ni idadi ndogo kabisa kuwahi kuonekana tangu Nigeria iliporejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka1999. Hasa katika Jiji la Lagos ambako watu milioni 6.1 walijiandilisha, ni watu milioni 1.1 tu ndio waliopiga kura.

Sababu kwanini watu wachache walishiriki katika uchaguzi huu ni kule kucheleweshwa kwa ghafla uchaguzi kwa wiki moja, alisema Hussaini Abdu, kiongozi wa Ushirika wa Kiraia ulioangalia uchaguzi huo. Mwanzoni uchaguzi huo ulipangwa ufanywe Februari 16. Sababu nyingine ni kwamba kadi za kupigia kura zilinunuliwa kwa mujibu wa bingwa huyo wa taaluma ya siasa.

Zaidi ya hayo, vyama vyote viwili vikuu vilitumia nguvu kutaka kufikia malengo yao ya kuwazuia wapinzani walio na haki ya kupiga kura wasiende kwenye vituo vya uchaguzi. Jumuiya ya Chunga Kura si tu ilipeleka waangalizi wa uchaguzi vituoni, lakini sambamba na jambo hilo ilikuwa inawauliza watu nje ya vituo namna walivyopiga kura. Kulikuwapo matatizo, alisema Abdu, lakini tunachukulia kwamba matokeo hayo ni ya kuaminika.

Kwamba watu wengi hawajashiriki kupiga kura ni ishara pia kwamba watu wamechoshwa na mtindo wa wanasiasa kutaka kujitajirisha wenyewe tu. Ukosefu wa ajira na kupanda ovyo bei za bidhaa kumewavunja moyo watu wengi. Huenda pia habari nzuri za ushindi wa Buhari ni kwamba anabakia madarakani mtu asiyekuwa na madoa ya ufisadi.

Jambo moja ni muhimu kulitambua. Chaguzi hazitatui tatizo. Nigeria itaendelea kukwama kwa vile wananchi, hasa vijana, hawana imani na wanasiasa. Viongozi wa dini pia wamepoteza imani ya vijana kwa vile wanajiambatanisha kwa karibu mno na wanasiasa. Si ajabu kuona vijana wengine wanaelekea kwenye siasa potovu za itikadi kali.

Kuchaguliwa tena Buhari kwa baadhi ya waangalizi wa mambo si jambo la kutuliza moyo. Na hata kama Abubakar angeshinda isitarajiwe kwamba mambo yangebadilika kuwa bora.  Mabadiliko yanayotakiwa ni namna Nigeria itakavyoongozwa na si juu ya nani ataiongoza nchi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles