Anna Potinus, Dar es Salaam
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeifungia kutoa huduma Bank M kutokana na kushindwa kufuata masharti waliyowekewa ikiwamo la ukwasi na hivyo mali na madeni ya benki hiyo yamehamishiwa kwa Benki ya Azania Bank.
Kaimu Gavana wa BoT, Dk. Bernad Kibese, amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“BoT inapenda kuutangazia umma kwamba imeamua kuwa mali na madeni ya Benki M yatachukukiwa na mtu mwingine ambaye ni Azania Bank Limited, kama ufumbuzi wa matatizo ya benki hiyo,” amesema Dk.Kibese
Aidha, amesema BoT haitasita kuingilia kati pale itakapoona benki yoyote inaelekea pabaya, pia amewataka wateja wote wenye madeni kuendelea kuyalipa kulingana na mikataba yao.
“Wateja wenye amana watatangaziwa tarehe ya kuanza kupata huduma za kibenki kupitia Benki ya Azania, na wale wenye mikopo wanatakiwa kuendelea kulipa mikopo hiyo kwa mujibu wa mikataba yao na Benki Kuu italisimamia hilo,” amesema Dk. Kibese.