Na KAHINDE KAMUGISHA – NGARA
WANAFUNZI watano wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Kihinga iliyoko Ngara mkoani Kagera, wamefariki dunia na wengine 43 kujeruhiwa baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu la kurushwa kwa mkono.
Miongoni mwa waliojeruhiwa na bomu hilo, ni mwalimu aliyetambulika kwa jina la Polycarp Clement.
Tukio hilo limetokea jana wakati wanafunzi hao wakiingia darasani.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa lilitokea jana saa 2:30 asubuhi wakati wanafunzi hao wakiwa kwenye foleni ya kuingia chumba cha darasa kufanya mitihani ya kumaliza muhula wa pili inayoendelea.
Ilielezwa kuwa wakiwa katika foleni hiyo, baadhi yao walikuwa wameshikilia vyuma chakavu mkononi, ambavyo huenda kuviuza eneo jirani na shule wakati wa mapumziko.
Mlipuko huo, ulitokea katika moja ya vyuma chakavu vilivyokuwa vimebebwa na wanafunzi hao.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Olomi, alisema chanzo cha tukio hilo ni vyuma chakavu vilivyobebwa na wanafunzi, ambavyo huuzwa eneo la jirani na shule, umbali wa mita 50.
“Hawa wanafunzi wana kawaida ya kwenda shuleni na vyuma chakavu kwa ajili ya kuviuza… kuna mnunuzi ambaye huwapatia madaftari, sasa leo (jana), kuna mwanafunzi alikuwa na vyuma hivyo bila kujua kama amebeba bomu na ghafla lililipuka.
“Kitendo cha kuuza vyuma chakavu ni kosa, mnunuzi wa vyuma hivyo anatafutwa na polisi… mwanafunzi aliyekuwa na vyuma hivi amepoteza maisha katika tukio hili, lakini mzazi wake tunamshikilia kwa ajili mahojiano zaidi,” alisema.
Kamanda Olomi, aliwataja wanafunzi waliofariki dunia katika tukio hilo kuwa ni Juliana Trasisi (14), Evart Theonas (12), Edson Bigilimana (12), Miburo Gabriel (12) na Tumsifu Ruvugo (8).
Naye Kamanda wa Kikosi cha Kulinda Mipaka cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Wilaya ya Ngara, Meja T. R. Mutaguzwa, alisema bomu hilo lilikuwa na vipande 36 na endapo lingelipukia ndani ya darasa, lingesababisha madhara makubwa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kibogora, Adronis Bulindoli, alisema wanafunzi watatu walifariki dunia hapo hapo eneo la tukio, wengine walipoteza maisha wakiwa njiani wakati wanakimbizwa Hospitali ya Misheni ya Rulenge kupatiwa matibabu.
Alisema tayari polisi wa kituo kidogo cha Bugarama na maofisa wa JWTZ wapo eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Erick Nkilamachumu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa madaktari wanafanya kila linalowezekana kuokoa maisha ya majeruhi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Rulenge, Goleth Francis, alikiri kupokea majeruhi 24 wakiwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao, wawili wakipoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini.