Anna Potinus
Rais John Magufuli amesema kuwa ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imeshikiliwa nchini Canada imeachiwa na kwamba Watanzania watatangaziwa siku ya kwenda kuipokea ndege hiyo.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Desemba 12, alipokuwa akifungua semina ya wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho Taifa (NEC) iliyofanyika Jijini Mwanza.
“Kwa taarifa tu ndege yetu iliyokuwa imeshikiliwa nchini Canada imeachiwa kwahiyo mtatangaziwa tarehe ya kuipokea na mtaipokelea hapa Mwanza,” amesema Rais Magufuli.
Baada ya ndege hiyo kukamatwa Waziri wa Mambo ya nje, Profesa Palamagamba Kabudi alisema aliyesababisha kukamatwa kwa ndege hiyo ni rais wa nchini Afrika Kusini, Hermanus Steyn ambaye alishawahi kuizuia ndege aina ya Airbus A220-300 kuondoka nchini humo Agosti mwaka huu hadi pale mahakama ilipoamuru ndege hiyo kuachiwa.