AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM
LICHA ya kusababisha ajali na madhara makubwa kwa watumiaji wake, na waendeshaji biashara ya pikipiki maarufu kama bodaboda imetajwa na taasisi nyingi kuwa ni biashara inayolipa kwa wawekezaji na inatoa ajira kubwa kwa idadi kubwa ya vijana nchini Tanzania; na sasa inataka kujiongeza kwa kuwa na benki yao yenyewe. Hii ni habari njema kwa kila mpenda maendeleo.
Ajira hiyo ya udereva wa bodaboda inawawezesha vijana kujipatia kipato kinachowasaidia kuendesha maisha yao na familia zao, kwa sasa ni shughuli maarufu sana barani Afrika kwani kila uendako huwezi kukosa huduma hiyo hapa barani Afrika.
Mbali ya kuwa usafiri kwa njia ya pikipiki ni rahisi pia ni wa haraka zaidi ukilinganisha na gari au bajaji na hivyo kuongeza maswali maisha yangekuwaje bila bodaboda.
Bodaboda ina uwezo wa kukwepa msongamano wa magari kwa hapa nchini hasa jijini Dar es Salaam kwa kujitahidi kuvunja sheria bila kukamatwa ingawa mwendo kasi wa bodaboda unahatarisha maisha ya watumiaji wa usafiri huo pendwa kwa vijana.
Hata hivyo baada ya kuonja tamu sasa waendesha bodaboda wamekuwa na mpango wa kuungana ili kuendelea kukuza biashara hivyo kwa ajili ya kupata faida zaidi kwani wanajua umoja ni nguvu.
Miongoni mwa mipango hiyo mahsusi kwa Boda boda za Dar es Salaam ni kuanzishwa kwa benki yao ambayo itaendeshwa na kusimamiwa na bodaboda wenyewe.
BODABODA DAR
Nchi nzima Dar es Salaam ndiko kwenye boda boda nyingi ingawa idadi yao haijulikani kwa sasa na juhudi inafanywa kupata takwimu sahihi lakini inakisiwa kuwa zaidi ya 50,000.
Mwenyekiti wa chama cha madereva na wamiliki wa pikipiki Mkoa wa Dar es salaam (CMPD) Michael Masawe amesema chama hicho kimeanza mchakato wa kufungua benki kwaajili ya madereva pikipiki maarufu kama bodaboda.
Akizungumza na MTANZANIA alisema kwa sasa wamesajili madereva 50,000 kwa mkoa wa Dar es salaam ambapo wapo katika mchakato wa kuimarisha kanzi data yao (database) ili kuangalia njia sahihi ya kuanzisha mfumo wa benki husika.
“Kwa sasa tumenza mchakato wa kuanzisha benki ya madereva bodaboda kwa mkoa wa Dar es salaam,madereva katika Mkoa huu ni wengi na mpaka sasa tumesajili 50,000 hapo bado kuna wengine hawajasajiliwa hata hivyo kwa sasa tunaimarisha mfumo wa kanzidata ili tujue idadi kamili,”anasema Massawe.
Masawe anasema mpango huo wa kanzidata utakaoudwa ni kwa kila dereva wa pikipiki atatoa Sh.500 kila siku kwaajili ya kuhifadhiwa kwenye benki hii ili itasaidia baadaye kupata mkopo nafuu na kuweka akiba kwaajili ya kesho yao.
“Katika mpango huu tutahusisha kwa kila dereva pikipiki kutoa Sh 500 kwa kila siku kwaajili ya kuhifadhiwa kwenye benki hiyo tumeona ni njia rahisi kwao kuweza kuchangia na benki hiyo itafuata mifumo yote ya kibenki,”anaeleza Massawe.
MADEREVA BODABODA
Kwa upande wake mmoja wa madereva bodaboda kituo cha Sinza Evod Pius anasema mpango huu ni mzuri kwao utasaidia kuweka akiba, kupata mkopo kupitia kazi yao, kurahisisha maendeleo kwa wamiliki na madereva na inafanya kazi yao kuheshimika katika jamii.
“Tunafurahi kwa mpango huo itatusaidia sisi kuwa na akiba kwa maisha ya baadae sio hilo tu kwani tutapata mkopo hii itasaidia kuboresha maisha yetu sisi madereva pia wamiliki na pia kujenga imani Kwa kuwa kazi hii sio ya kihuni hivyo itaheshimika kama kazi zingine “Anasema Pius.
Anaongeza, “Kwa muda mrefu tumekuwa hatupati mikopo kutoka kwa benki zingine lakini tukiwa na benki yetu tutaweka mifumo mizuri kwaajili ya kuboresha maisha yetu hivyo ni jambo zuri sana tunafurahi.
Naye Abel James dereva bodaboda mwingine anasema wanawapongeza viongozi wao kwani hatua hiyo ni nzuri kwao na kuomba mpango huo ufanyiwe kazi haraka kwani kupitia hapo hata serikali itajiingizia kipato.
“Viongozi wetu wanamawazo mazuri binafsi napongeza hatua hiyo tunachokiomba mpango huo ufanyiwe kazi haraka itanufaika hata baadaye tunatumia benki yetu vizuri na tukotayari kuichangia,”alisema James.
MTAALAMU WA UCHUMI
Mtaalamu na nguli wa masuala ya uchumi Profesa Haji Semboja,anasema kutokana na mfumo wa utafiti wa fedha unatoa huduma mbalimbali za kifedha inakubalika kuwepo kwa mfumo kama huo kwani hata katika nchi zilizoendelea mfumo huo upo hivyo wanaweza kufanikiwa.
“Inakubalika kuhifadhi fedha za bodaboda kwa mfumo wa Kibenki, katika nchi zilizoendelea huduma za kifedha ndogo (microfinance) zinakubalika kulingana na mifumo ya utafiti wa kifedha hivyo watafanikiwa kutoka kwa kuwa madereva bodaboda wengi ni vijana na wanaelimu ya kati,”alisema Semboja.
Semboja anasema kama kuna watu wengi na mtaji benki inaweza kujilinda na kuhudumia watu kikamilifu hivyo bodaboda kama wataendelea kuongezeka kunauwezekano wa kupata mtaji mkubwa zaidi.
“Kuwa na idadi kubwa ya madereva bodaboda ni kitu kizuri kwani benki inaweza kupata mtaji mkubwa haraka na wanaotaka zaidi utakumbuka mfano wa benki ya CRDB ilikuwa ya wakulima tu lakini mpaka sasa imeimarika na kutumika na watu wote,”alieleza Semboja.
Hata hivyo anawataka madereva bodaboda kuona kazi hiyo kama kazi zingine na kuwataka wajiendeleze kielimu ili wapate ujuzi waweze kuiweka mikakati, sera za kimaendeleo na kufuata sheria za usalama barabarani.
UTARATIBU WA BENKI KUU
BoT ni msimamizi wa masuala yote ya biashara ya fedha nchini na walipoulizwa walisema hawana wasiwasi juu ya wao bodaboda kuwa na benki ila inabidi wafuate taratibu, kanuni na masharti ya biashrara hiyo kwani iko wazi ingawa sio rahisi kwani haina njia ya mkato bali wafuate mahitaji ya sheria wakati wote kwani benki ni mapahala amabapo watu huweka amana zao na hivyo lazima kuwe na usalama wa hali ya juu. Weledi na uaminifu ni msingi wa biashara hiyo.
Kanuni za benki kuu katika uanzishwaji wa benki au taasisi ya kifedha hapa nchini unazingatia kuwasilisha habari hizi kwa usimamizi wa benki kama ilivyoainishwa hapa chini.
1. Barua ya Maombi katika muundo uliowekwa.
2. Mapendekezo ya Mkataba wa Chama (haujasajiliwa na Msajili wa Makampuni).
3. Makala yaliyopendekezwa ya Chama (bila kusajiliwa na Msajili wa Makampuni).
4. Ushahidi wa Upatikanaji wa Mfuko wa Uwekezaji kama Msingi wa Taasisi Iliyopendekezwa e.g kibali cha benki.
5. Orodha ya Wafanyabiashara husika / Washirika na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na maafisa wengine wakuu.
Karatasi ya Taarifa ya Kila Mshiriki / Msajili na Kila Mwanachama aliyepangwa wa Bodi ya Wakurugenzi, na Afisa Mkuu.
7. Uthibitisho wa Uraia wa Kila mshiriki / Msajili na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mkuu. Hii ni pamoja na wasifu wa Kila mshiriki (Curricula Vitae (CV), Fotokopi ya Kurasa Tano za Pasipoti, Picha ya Pasipoti ya kila mhusika na Historia yake.
8. Karatasi ya Hesabu na Taarifa ya Mapato ya Kila Incorporator / Msajili na Kila Mwanachama Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi na Afisa Mkuu ambaye anajihusisha na Biashara.
9. Hati za kuthibitishwa za Kurudi kwa kila Mtokezaji / Msajili na kila Mwanachama aliyependekezwa wa Bodi ya Wakurugenzi na Afisa Mkuu (pamoja na ratiba zinazoambatana na taarifa za kifedha) zilizojazwa Katika Miaka mitano iliyopita na Ofisi ya Kodi ya Mapato (TRA) kwa Mapato ya Kodi ya Mapato.
10.Ufunguzi wa Kodi kutoka Ofisi ya Kodi ya Mapato
11.Taarifa kutoka kwa Watu wawili (sio jamaa) Kujiunga kwa Tabia nzuri ya Kimaadili na Uwezo wa kifedha wa Waingizaji / Washirika na Wakurugenzi waliopendekezwa na Maafisa Wakuu.
12.Mipango ya Biashara kwa miaka minne ya operesheni ikiwa ni pamoja na Mkakati wa Ukuaji, Mpango wa Kueneza Tawi, Sera ya Malipo ya Kugawanya na Programu ya Maendeleo ya Kazi kwa Wafanyakazi, Bajeti za Mwaka wa Kwanza Lazima Pia Uwe pamoja
13.Mipango ya Mikopo ya Kila Mwaka kwa Miaka minne ya Uendeshaji.
14.Taarifa ya Mapato ya Mwaka kwa Miaka minne ya Uendeshaji.
15.Taarifa zilizopangwa kwa Mwaka wa Fedha za Fedha kwa miaka minne ya operesheni.
16.Majadiliano ya Faida za Kiuchumi ambayo yamefanywa na Nchi na Jumuiya Kutoka Taasisi ya Benki / Taasisi ya Fedha.
MAFANIKIO YA BODABODA KENYA
Nchini Kenya wakati bodaboda wa Tanzania wakijipanga kuendelea kwenye ukombozi kiuchumi, Takwimu za Chama cha Waunda Pikipiki Kenya (MAAK), wamebainisha kuwa, kuna takribani pikipiki 600,000 katika barabara za Kenya, kila moja ikiingiza wastani wa Shilingi za Kenya 1,000 kwa siku, sawa na Sh 20,000 za Tanzania kwa siku.
Na kutokana na takwimu hizo, tafsiri iliyo rahisi ni kwamba, Sh milioni 600 za Kenya hupatikana kutokana na idadi hiyo, sawa na Sh bilioni 219 za Kenya kwa mwaka.
Mwenyekiti wa MAAK, Isaac Kalua anafafanua kuwa, wastani wa watu wanane wanaendesha maisha yao kwa kutegemea pikipiki moja inayofanya kazi kila siku. Kwa ujumla, kwa mujibu wa Kalua, pikipiki hizo zinalea takribani watu milioni 4.8.
Kama ilivyo kwa Kenya, nchi nyingine ya Afrika Mashariki ya Uganda, waendesha bodaboda wameunda umoja wenye lengo la kuwaweka pamoja zaidi na hivyo kupiga kasi kimaendeleo.
MAPUNGUFU YA MRADI
Uchunguzi unaonesha kuwa Mfumo wa uongozi na oganizesheni ya Boda Boda nchini bado ni dhaifu kwani sio chombo cha kitaifa na hakijasajiliwa na hivyo maoni hayo hayana ushahidi wa kuungwa mkono na wengi zaidi ya kuwa viongozi waliotoa kauli ni wale wa Dar es Salaam pekee ingawa kuna uongozi kila mkoa na hivyo kuhitaji majadiliano ya kina zaidi. Kilichotayari hadi sasa ni wazo ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi kwa mpangilio unaostahili na ukizingatia mahitaji halisi ya sekta hiyo ya usafirishaji yaani ni mikopo kwa masharti yaliyo nafuu na kuwa na maduka ya wanachama ambayo yatauza vipuri kwa bei nafuu. Hakuna uwazi ni nani mhusika kwani kuna kuchanganya kati ya madereva na wenye vyombo na hivyo inatakiwa ijulikane nani ni mwanachama kwani ukiwachanganya hawa wenye masilahi yanayo pingana kuna hatari ya kukosa mwelekeo na hivyo badala ya kuanza na benki ingeanza kwanza usajili wa Chama ambao una sura ya kampuni yaani board corporate na inatawaliwa na umiliki wa dhamana yaani limited by gurantee na sio by limited by shares.
Mwishooo….