32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Bila suluhu mzozo wa Kashmir hakuna amani India, Pakistan

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA

MOJA ya vichwa cha habari vinavyotawala anga ya kimataifa katika wiki za karibuni ni mgogoro baina ya mataifa mawili jirani lakini hasimu; Pakistan na India.

Mgogoro huo ulioshuhudia upotevu mkubwa sana wa maisha na mali katika pande hizo mbili, ni moja ya ile migumu kabisa duniani, isiyoonesha dalili za kumalizika katika miaka hata miongo ya karibuni.

Awali mataifa hayo pamoja na Bangladesh, ambayo ilimeguka baadaye kutoka ubavuni mwa Pakistan yalikuwa taifa moja kubwa la Bara Hindi likitawaliwa na ukoloni wa Uingereza. Baadaye yakaja kugawanyika baina ya mataifa mawili kwa misingi ya kidini; Uhindu (India) na Uislamu (Pakistan).

Yamekuwa yakipigana kuwania jimbo la Kashmir lililopo baina ya mpaka unaozitenganisha kwa zaidi ya miaka 70 sasa ikiwamo vita tatu kamili.

Katika mgogoro wa sasa kama ilivyo mingine mingi ya miongo ya karibuni imechochewa na wanamgambo wanaoendesha shughuli zao eneo hilo la India na Pakistan.

Lakini Pakistan imekuwa ikikana kuhusika nayo wala kuwalinda wanamgambo hao, ambao katika mgogoro wa sasa Februari 14, waliendesha shambulio la kujitoa mhanga lililoua askari 40 wa India.

India ikalipa kisasi kwa kuendesha mashambulizi makali ya anga huku Pakistan ikitungua helikopta mbili za India na kumkamata rubani mmoja katika eneo la Kashamiri linalodhibitiwa na taifa hilo, ikiwa ni siku moja baada ya India kusema jeshi lake lilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya kambi ya wanamgambo wa upande wa Pakistan.

Na katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na Pakistan, afisa wa serikali Umar Azam alisema wanajeshi wa India waliojihami kwa silaha nzito wamekuwa wakivilenga vijiji vya upande wao karibu na mpaka huo na kusababisha vifo vya watu kadhaa akiwamo mtoto mmoja wa kiume na kuwajeruhi watu wengine watatu.

Ameongeza kwamba nyumba kadhaa pia zimeharibiwa na mashambulizi hayo ya mabomu yaliyofanywa na wanajeshi wa India.

Kufuatia masaa machache ya utulivu, mashambulizi ya mabomu na ya kutumia silaha ndogo ndogo yalianza tena Jumamosi.

Taarifa ya jeshi la Pakistan imesema raia wao wawili waliuawa na wengine wawili walijeruhiwa katika mapigano hayo.

Jeshi la India lilidai wanajeshi wa Pakistan walivishambulio vituo vyao kadhaa katika eneo hilo linazozitenganisha pande mbili za Kashmir.

Vurugu zinazoendelea hivi sasa ni mbaya zaidi kushuhudiwa katika mvutano ulionza kufukuta chini kwa chini tangu 1999, pale jeshi la Pakistan lilipotuma kikosi cha ardhini katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India.

Mwaka huo huo pia ndege ya kijeshi ya India iliidungua ndege ya jeshi la anga la Pakistan na kupelekea watu wote 16 waliokuwamo kufa.

Katika mapigano ya sasa, maelfu ya watu wa pande zote mbili za Kashmir wameyahama makazi yao na kukimbilia katika makazi ya muda yanayosimamiswa na serikali zao huku wengine wakikimbilia kwa jamaa zao wanaoishi katika maeneo yaliyo salama zaidi wakikimbia eneo linazozitenganisha ambalo limegawanywa kwa uzio wa seng’ng’e na minara ya uangalizi.

Eneo hilo liko katikati ya misitu pamoja na mashamba ya mpunga na mahindi.

Kijiografia Kashmir ni bonde kubwa la mto Jheam lenye rutuba kati ya Himalaya ya Juu na milima ya Pir Panjal.

Katika karne ya 19 bonde liliunganishwa na maeno jirani ya Jammu na Ladakh likiwa na jumla ya ukubwa wa kilomita mraba 222,236 penye milima na chanzo cha Mto Indus (Hindi) hata hivyo eneo hili liligawiwa 1947.

India hulitambua kama jimbo la kujitawala ndani ya shirikisho la India likitumia jina la kihistoria ‘Jammu na Kashmir’.

Baada ya kugawanywa, Kashmir inayodhibitiwa na India ikawa na eneo la kilomita mraba 101,387 na wakazi milioni 10.1 huku sehemu ya Pakistan ikijulikana kama Asad Kaschmir, yaani ‘Kashmir Huru’ eneo lake likiwa na ukubwa wa kilomita mraba 83.888 na wakazi milioni 1.3.

Huku pia sehemu ya China ni Aksai Chin. Eneo hili ni jangwa baridi la chumvi lenye ukubwa wa kilomita mraba 38,000 na wakazi wachache sana.

Katika historia ya eneo hilo hadi 1947 sehemu zote za Kashmir zilikuwa eneo la dola la watemi yaani ‘maharaja’ wa Jammu na Kashmir, chini ya utawala wa Uingereza.

Awali mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu duniani na kiongozi wa harakati za uhuru wa India, ama tuseme baba wa taifa la India, Mahatma Gandhi alipinga kuligawa Bara Hindi kuwa misingi ya kidini.

Yeye na vuguvugu lake la Indian National Congress waliendesha kampeni ya kuitaka Uingereza iondoke katika ardhi yao ili wajitawale wenyewe.

Lakini vuguvugu la Muslim League likiongozwa na Muhammad Ali Jinnah walitaka Bara Hindi ligawanywe kwanza kabla ya Uingereza kuondoka.

Gandhi alijitahidi kuleta mshikamano baina ya Congress na Muslim League katika upatikanaji wa uhuru wa taifa lao na upatikanaji wa suluhu ya mgawanyo wa kidini uliopo humo.

Badala ya kugawa Bara Uhindi katika mataifa mawili kwa mzingatio wa dini, alipendekeza maeneo yenye watu wengi wa dini moja yawe wilaya zinazojiendesha.

Lakini Jinnah alikataa pendekezo hilo na akaitisha ‘Siku ya Maamuzi’ Agosti 16, 1946, kuwahamasiaha Waislamu waunge mkono wazo lake la kuigawa Bara Hindi baina ya taifa la Waislamu na wasio Waislamu.

Harakati hizo zikapelekea machafuko yaliyoua maelfu ya Wahindu na Waislamu.

Mwishowe Uingereza walichoka habari za vuguvugu la kudai uhuru wa India, hivyo ikitokea kupigana vita kali na chovu ya pili ya dunia, Serikali mpya ya Chama cha Labour ya Uingereza iliamua kuipa India uhuru wake. Hivyo Agosti 14/15, 1947 utawala huo ulikoma.

Ndani ya India kwenyewe fitina ziliendelea tena kwa kasi zaidi juu ya nafasi ya Waislamu katika taifa jipya, huku sehemu kubwa ya Waislamu wakidai kugawiwa nchi yao.

Hivyo, Bara Hindi iligawanywa katika nchi mbili za India na Pakistan katika uamuzi uliochagizwa na Jinnah kutoka Pakistan na Wahindu wa India wakiongozwa na Jawaral Nehru.

Wakati Serikali ya Uingereza ilipotoa uhuru, sheria yake pamoja na mambo mengine ilisema maeneo penye Waislamu wengi yangekuwa upande wa Pakistan na maeneo penye Wahindu wengi upande wa India.

Kashamir ikapewa uhuru wa kuchagua wapi ijiunge baina ya pande hizo mbili.

Lakini mtawala wa eneo hilo, yaani Maharaja Hari Singh wa Jammu na Kashmir  alijaribu kutetea uhuru wa utemi (eneo lake kimila) wake bila kujiunga na upande wowote.

Hata hivyo, Pakistan ilichochea upinzani ikadai ya kwamba eneo hili lenye Waislamu asilimia 70 ya wakazi ilipaswa kuwa sehemu yake.

Alipoleta upinzani ndipo aliposhambuliwa na wanamgambo wa Kiislamu waliosaidiwa na kuongozwa na jeshi la Pakistan. Baada ya kuona anaelekea kushindwa katika mapigano hayo, maharaja alitangaza kujiunga na Shirikisho la India akaomba msaada wa kijeshi wa India dhidi ya Pakistan, hali hiyo ikachochea vita.

Oktoba 1947 vita ikafuatia kati ya nchi zote kugombea jimbo hilo, maelfu ya watu waliuawa.

Vita vikaongeza uadui na watu mamilioni walifukuzwa yaani Wahindu kutoka Pakistan na Waislamu kutoka Uhindi.

Ghandhi aliwalaumu wanasiasa kusababisha migogoro hiyo. Alifunga kula chakula kama masharti ya kutaka kumalizwe mgogoro huo akitangaza alikuwa tayari kufunga hadi kifo wasipopatana.

Ilikuwa ni Januari 30, 1948 Gandhi alipigwa risasi na kuuawa alipokuwa akitembea katika bustani ya nyumba yake mjini New Delhi.

Muuaji wake alikuwa Mhindu wa kundi lililofuata itikadi kali. Kijana huyo alikasirishwa sana na hatua za kuwapatanisha Waislamu na Wahindu akaamini kuwa Gandhi alikuwa msaliti wa dini ya Uhindu.

Vita ilipiganiwa kati ya Oktoba 1947 hadi mwisho wa mwaka 1948. Tokeo lake lilikuwa mgawanyiko wa Kashmir kwenye mstari wa mapigano baina ya nchi mbili za Pakistan na India. Kashmir imesababisha tayari vita tatu za 1947, 1965 na 1999 kati ya nchi hizi.

Imekuwa pia chanzo cha machafuko kadhaa ndani ya India hasa eneo hilo la Kashmir, kwa vile eneo hilo lenye ambalo asilimia 60 ni Waislamu na kulifanya jimbo pekee la India lenye Waislamu wengi zaidi nchini humo.

Machafuko ya mara kwa mara eneo hilo kulinganisha na Pakistan ni kwa vile hawapendi kuongozwa na India yenye Wahindu wengi badala yake wanataka ama wajitenge au kuungana na Pakistan kwenye Waislamu wengi.

Kwa usuluhishi wa Umoja wa Mataifa, nchi hizo mbili zilikubaliana kuruhusu Wakashmiris kuamua hatima yao wenyewe, lakini hilo haikufanyika kwa sababu ilitakiwa kwanza kuondoka kwa majeshi ya mataifa yote mawili kutoka eneo hilo. Hilo halikutelekezwa mwongo mmoja sasa.

Mamlaka za India zilitaka kuonesha zinatoa haki kwa Waislamu katika taifa lisilo na dini, lakini Kashmir pia ni muhimu kwa utambulisho wa Pakistani kama nyumbani kwa Waislamu baada ya kugawanywa mwaka 1947.

Hisia za chuki baina ya wananchi wa pande mbili bado zingalipo hadi sasa na zilishuhudiwa na shangilia ya raia wa India na Pakistan wakati zikishambuliana katika mgogoro wa sasa.

Na kwa sababu hiyo, uchaguzi mkuu wa mwaka huu nchini India umechangia kukuza mgogoro huo kama ilivyoshuhudiwa na namna Modi alivyoitikia katika kujibu shambulio la Februari 14.

Mashambulizi makali ya anga aliyoamrisha yamefanikiwa kupaisha taswira yake kama kiongozi imara asiyeyumba katika kuilinda India na tayari wanaomuunga mkono wameitumia vyema fursa hiyo.

Rais wa chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP), Amit Shah aliandika katika akaunti ya tweeter wiki iliyopita kwamba kitendo hicho kinaonesha India iko salama chini ya uongozi wenye nguvu na wepesi kimaamuzi wa Modi.

Mbali ya India, Pakistan pia imetumia fursa hiyo vyema kwa kutungua helikopta mbili pamoja na kumkamata rubani, ambaye tayari imemuachia kuonesha namna inavyoweza kulinda anga lake dhidi ya inachokiita uchokozi wa India.

Wakati Pakistan ilipotungua ndege za India, baadhi ya Wapakistan walimiminika mitaani kushangilia huku wengine wakipeana vinywaji na vitu vitamu kama pipi kadhalika walifanya Waindia wakati jeshi la India lililipoendesha mashambulio ya anga.

India inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Mei mwaka huu, ambapo Waziri Mkuu Narendra Modi aliahidi kurekebisha uchumi na kuzalisha ajira pamoja na kuwakabili maadui wa India, bila shaka akiilenga zaidi Pakistan.

Modi amekuwa akishughulika vilivyo na matatizo ya uchumi ikiwamo uhaba wa ajira na kuanguka kwa vipato vijijini, licha ya ukuaji wa uchumi.

Na chama chake cha BJP bila kutarajia kilifanya vibaya katika chaguzi za majimbo Desemba mwaka jana na kuibua hofu ya uwezekano wa kupata matokeo mabaya katika uchaguzi wa kitaifa mwaka huu.

Licha ya kwamba Pakistan inabeba lawama kwa kushindwa kuwadhibiti wanamgambo walio upande wake wanaoendesha mashambulizi ya mara kwa mara upande wa India, wachambuzi wengi wa mambo wanaamini uhusiano wa mataifa haya mawili ambao hutulia na kuvurugika safari hii umekuwa mbaya zaidi kipindi cha Modi tangu alipoingia madarakani mwaka 2014.

Wanaamini Modi ameichukulia Kashmir kama suala la kiusalama na kuruhusu hali ya kisiasa kudhoofu vibaya tangu miaka ya 1999.

India na Pakistan zilikubaliana kusitisha mapigano mwaka mwaka 2003 baada ya miaka mingi ya mwagaji damu mpakani.

Katika makubaliano hayo Pakistan baadaye ikaahidi kusitisha ufadhili kwa wanamgambo katika eneo lake na India ikitatoa ofa ya msamaha kwa wafungwa wa Pakistan.

Lakini mwaka 2014, serikali mpya ya India (Modi) ikaingia madarakani na kuahidi msimamo mkali dhidi ya Pakistan, lakini pia ikionesha utayari wa mazingumzo ya amani.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif, pia alihudhuria sherehe za kuapishwa kwa Modi mjini Delhi.

Mzozo uliibuka Septemba 2016, wakati wanamgambo wenye silaha waliposhambulia kambi ya jeshi la India karibu na mpaka unaotenganisha Kashamir zinazodhibitiwa na mataifa haya ujulikanao Line of Control (LoC) na kuua askari wa India  19 katika kile kilichokuwa shambulio baya kwa majeshi ya India kipindi cha miongo kadhaa.

Na baadaye mwezi huo askari wawili wa Pakistan wameuawa baada ya mapigano na askari wa India mpakani hapo. India ilidai kwamba iliendesha mashambulio eneo hilo kulenga magaidi waliopo katika Kashamir ya Pakisyan.

Modi akafuta ziara yake nchini Pakistan kwa mkutano wa kikanda mwaka 2017. Tangu hao hakuna maendeleo yoyote ya mazungumzo baina ya majirani hao.

Mtiririko huo wa matukio wa karibuni pamoja na umwagaji damu ulioshuhudiwa wakati wa maandamano ya mitaani katika Kashmir a India mwaka 2016 ukapoteza kabisa matumaini ya amani ya kudumu eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles