24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

BIFU LA DUMA, GABO KATIKA SURA TOFAUTI

 

 

Na JOSEPH SHALUWA

WAKATI soko la filamu za Kibongo likiendelea kudorora, kumeibuka kituko kwenye tasnia hiyo. Kichekesho hicho ni kinachoitwa bifu la Duma (Daudi Michael) na Gabo (Salim Ahmed). Kwa hakika ni kituko.

Kwamba, watu waache kufikiria namna ya kutoka kwenye matope, tuanze kuwajadili wao. Katika mitandao ya kijamii, upepo umebadilika na wanajaribu kukuza hiki kinachoitwa bifu.

Nilianza kufuatilia huu mchezo tangu mwishoni mwa Septemba, mwaka jana. Sikutia neno. Wiki hii tena wameibuka kwa sura ileile. Nimeona kuna haja ya kuandika kuhusiana na jambo hili. Hapa nitaelezea kwa kadiri nilivyoelewa bifu hili katika sura tofauti.

GABO ZIGAMBA…

Namfahamu Gabo muda mrefu kisanii. Nimeanza kumfahamu zaidi alipoanza kucheza sinema za Jerusalem Film Company ya mwigizaji Jacob Stephen ‘JB’. Tangu nimeona kazi yake ya kwanza, nimekuwa nikifuatilia kazi zake kwa karibu.

Niseme ukweli, ni msanii ambaye niliona uwezo wake tangu mapema kabisa. Nilipomuona kwenye Fikra Zangu, baadaye Majanga nikampa maksi zangu 90 katika uwezo wake wa kuigiza.

Anafanya kazi nzuri, mapungufu ya hapa na pale yapo kama msanii hasa kutokana na mazingira ya kazi hapa  Bongo. Lakini kwa ujumla wake, unapotaja wasanii 10 wa kiume wenye uwezo, jina la Gabo kamwe huwezi kuliweka kando.

Namfahamu kama msanii anayejitambua, asiyependa makundi, mwenye ndoto za kufika mbali, anayeishi kwenye malengo na asiyekata tamaa. Huyo ndiye Gabo ninayemfahamu.

DUMA NAYE…

Nilipomuona Duma kwa mara kwanza kwenye Tamthilia ya Siri ya Mtungi, nilisema yes! Bongo Muvi imelamba dume. Tangu hapo nikaanza kumfuatilia. Kwa ujumla niliona uwezo mkubwa wa msanii huyu.

Hata nilipomfuatilia kwenye Tamthilia nyingine za Nyota na Huba nilijiridhisha pasipo shaka kuwa kijana kazi anaiweza.

Kimsingi Duma amekuja na moto na kiukweli hajawahi kupoa tangu alipoanza kukubalika kwenye game. Ni msanii wa aina yake, mwenye uwezo wa kufikisha mbali sanaa na sanaa ikabadilisha maisha yake.

SURA ZA BIFU LENYEWE

Natazama bifu lao katika sura mbili – la ukweli au la kupanga. Huenda wamekubaliana kufanya bifu ili wakubalike zaidi kwa mashabiki. Kama ndivyo, hii itakuwa kiki ya kipuuzi kuwahi kutokea.

Na mnufaika hapo atakuwa Gabo. Kama ni kweli, siyo kiki basi Duma anajiharibia mwenyewe! Nimemuona akiongea zaidi na social media, akitumia nguvu nyingi kumponda Gabo.

Anamsema kwa mengi. Mara hajui kuvaa, hana dili za nje ya nchi kama yeye. Anamwita Gabo ni virus na yeye ni anti virus! Anajisifu kwa safari za Kenya, Uganda na nchi nyingine za nje.

Anasema Gabo hatumii vizuri uaminifu anaoaminiwa na Watanzania kwa kutoa kazi nzuri kila wakati. Eti ana tuzo nyingi, lakini hajafanya kitu kikubwa. Iwe kiki au bifu la kweli, hapa Duma amechemka na anaharibu jina lake alilolisotea.

JB, Richie (Single Mtambalike) na Bishanga (Alen Raymond) kwa pamoja waliamua kukaa pembeni ya soko kwa muda mrefu, tena wakaanza kujishughulisha na kazi nyingine kabisa nje ya sanaa, lakini walipoamua kurudi waliingia kwa miguu miwili!

Richie ameendelea kuwa msanii mzuri mpaka sasa, kadhalika JB na Bishanga ambaye huonekana kwa nadra  kwenye filamu, lakini thamani yao haijawahi kushuka. Filamu nyingi siyo ubora katika kuigiza.

Kuandika script hakumthibitishi mtu kama msanii bora. Wapo waandishi wengi wa miswada ya filamu siyo waigizaji. Kuandika ni taaluma. Kuigiza hasa ni kipaji. Duma anachanganya madawa hapa iwe kwa kujua au  kutojua.

DUMA HAJAWAJUA MASHABIKI

Duma ajue kuwa thamani yake kwa mashabiki ni kubwa. Na kama walikubaliana na Gabo kuwa watengeneze kiki, atambue kuwa ameingizwa choo cha kike! Ni kiki itakayomgharimu badala ya kumpandisha.

Kwa tambo zake, kwamba anaigiza tamthilia za kimataifa, anaigiza na wasanii wa kimataifa, anajua kuvaa nk, mashabiki watatafsiri kama maringo, mwisho wake watamuonea huruma Gabo, kisha watamchukia (Duma).

Huo ndiyo ukweli. Kama basi haijapangwa, atambue kuwa jamii inamuona hivyo na muda mfupi ataona malipo ya anachokifanya. Kama ni dili avunje, maana ni hatari kwa sanaa yake.

Katika mtazamo wa kawaida; kwa Gabo ambaye amefanya kazi nyingi nzuri kama Bado Natafuta, Safari, Safari ya Gwalu na nyinginezo, tena akiwa na tuzo kibao mkononi ikiwemo ya kimataifa ya Sinema Zetu (SZIFF), kuingia kwenye vita ya maneno naye, tena ukiwa mzungumzaji zaidi wewe, lazima watu wataona una wivu.

Kwa namna yoyote ile, Duma ajiondoe kwenye hili tatizo ambalo kama halijampata, basi linamnyemelea.

TUJIKUMBUSHE YA RAY NA KANUMBA

Marehemu Steven Kanumba alikuwa na bifu la kisanii na swahiba wake, Vincent Kigosi ‘Ray’. Lile lilikuwa bifu la kibiashara kwelikweli. Walitengeneza bifu la maana na likawa na manufaa kwao wote.

Walikuwa na tambo kwenye kazi, lakini kwa maneno ya staha. Hakuna mahali popote tulipata kuwasikia wakigombana au kurushiana maneno yasiyo na staha. Walitambiana magari, walishindana kuagiza vitendea kazi nje na kazi bora.

Lakini mwisho wa siku, walikuwa wakikutana na kufanya kazi pamoja zilizozidi kuwapaisha kisanii (tukumbuke Oprah na Off-Side). Hivyo basi, kama Gabo na Duma wameamua kutengeneza bifu la kibiashara, wabadili sura.

Ama kama ni kweli wapo kwenye bifu, Duma aelewe kuwa litamtafuna yeye na kuzidi kumpandisha Gabo. Natamani ninachokiona kiwe ndoto. Kwa sababu ni halisi, basi ni hamu yangu kiishe mara moja. Turudi kwenye mstari wa kujadili mkwamo wa sinema zetu, siyo bifu za kuzidi kuua sanaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles