Na MWANDISHI WETU
BENKI ya Standard Chartered imeahidi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanawake wanapewa kipaumbele kwenye elimu ya jamii na masuala ya kifedha.
Benki hiyo imedhamini kongamano maalumu kwa wanawake lililofanyika kwa siku mbili, lenye lengo la kusaidia kuleta maendeleo kwa wanawake, ambalo limefanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, nchini Tanzania.
Kongamano hilo la siku mbili liliwakusanya pamoja wanawake viongozi katika fani mbalimbali, zikiwamo taasisi za kibenki, teknolojia, wafanyabiashara na mashirika ya umma pamoja na mashirika binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani, alisema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuwawezesha wanawake kupata mitaji ya kifedha.
Alisema benki hiyo imekuwa ikiwaelimisha wanawake kuhusu masuala ya fedha na uchumi, kutoa bidhaa maalumu za kibenki kwa ajili ya wanawake na pia kuwawezesha kupitia miradi yake ya kijamii.
Alisema wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi yoyote, hivyo wamejizatiti kikamilifu kuwawezesha kuwa na uhuru na uchumi na elimu ya fedha na kuweka akiba pia.
Aliongeza kuwa, hakuna taifa hapa duniani ambalo linaweza kuendelea bila kuwa na wanawake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Mabenki, Heidi Toribio, alisema mwanamke anayejiweza kiuchumi anasaidia siyo tu biashara yake, bali pia na familia yake na anakuwa mtaji mkubwa kwa jamii yake na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.