28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

BAVICHA WAMSHAMBULIA LOWASSA

Na TUNU NASSOR -DAR ES SALAAM

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha)  limesema limeshangazwa na kauli ya aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Edward Lowassa, kumsifia Rais Dk. John Magufuli.

Katibu Mkuu wa Bavicha, Mwita Julius amesema   suala hilo halijawahi kujadiliwa katika vikao vya chama hicho.

Kauli hiyo imetolewa siku mbili baada ya Lowassa kwenda Ikulu na kuzungumza na Rais Dk. Magufuli ambako kiongozi huyo alipongeza kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Julius  alisema wameshangazwa na kauli hiyo na kwamba ilikuwa yake binafsi na si msimamo wa chama hicho.

Alisema misimamo ya chama hicho  hujadiliwa kwanza katika vikao na ndipo hutolewa kwa umma na mwenyekiti au mtu yeyote aneyeteuliwa kuzungumza.

“Mjumbe wa Kamati Kuu unapataje ujasiri wa kuisifia serikali wakati taifa halijui mustakabali wake wa uchumi?

“Kuna tatizo la wabunge wa upinzani kufukuzwa bungeni, mwanasiasa Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi…kama chama tumeshangazwa!” alisema Mwita.

Alisema Lowassa kwenda Ikulu kuonana na Rais Magufuli kwao halina shida bali wanashangazwa na kauli   alizozitoa baada ya kufanya mazungumzo hayo.

Alisema iwapo Lowasa ataamua kuondoka katika chama hicho na kurudi Chama cha Mapinduzi (CCM) wao kama chama hawatamzuia bali watamtakia maisha mema huko aendako.

“Hatuhofu kama ataamua kurudi CCM kwa sababu  kama Chama tumepitia misukosuko mingi ikiwamo baadhi ya wanachama wetu kujitoa na kuanzisha vyama vingine na hata sasa viongozi wetu wanahamia huko,” alisema Julius.

Wakati huo huo, Baraza hilo limemjibu Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alivyomshambulia kwa maneno Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu akiwa bado hospitali.

Hivi karibuni Shaka alipinga kauli ya Lissu kuwa yeye siye mwanasiasa wa kwanza kushambuliwa na risasi.

“Tunamkumbusha kuwa Hayati Abeid Amani Karume ambaye aliuawa kwa kushambuliwa na risasi haikuwa sababu za siasa kwa kuwa hakuwa mpinzani wala mkosoaji wa serikali kama Lissu na hata hivyo washambuliaji walikamatwa na wengine kuuawa,” alisema Julius.

Akijibu mapigo hayo ya Bavicha, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema wao hawatapoteza muda kujibishana na Bavicha akidai hawana upeo wa siasa.

Akizungumza na MTANZANIA kwa   simu akiwa mkoani Singida, alisema wao kama vijana sasa wameamua kulinda heshima ya Rais na chama, katu hawako tayari kuona watu wanataka kuvuruga nchi.

“Nawashauri Bavicha wafanye tafakuri ya kutosha kama vijana wamshauri Mwenyekiti wao Mbowe na chama chao namna ya kukinusuru na kifo kwa sababu  chama kimeshawashinda na sasa kinachungulia kaburi,” alidai Shaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles