24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

BASHE ATAKA MGOMBEA CHADEMA APEWE ULINZI YASIJIRUDIE YA KINONDONI

 
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam



Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ulinzi wa kutosha kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Asia Msangi ili kuondoa uzushi kuwa mgombea huyo anataka kutekwa.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni za jimbo hilo uliofanyika Mziga Mwanagati, jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Septemba 10, Bashe amesema kuna taarifa zimetolewa na watu wa Chadema wakidai wamepata taarifa kuwa mgombea wao atatekwa, hivyo ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama vikahakikisha vinamlinda.

Bashe amesema si vema kupuuza maneno hayo kwani wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni walipuuza yakatokea maafa.

“Nimesikia wakitoa hoja kuwa CCM wanataka kumteka mgombea wao, vyombo vya ulinzi naomba mtoe ulinzi huyu dada alindwe kuanzia nyumbani kwake, kwenye gari na kwenye kampeni ili isije ikafika mahali wakaanza kusema ametekwa,” amesema Bashe.

Pamoja na mambo mengine, Bashe amesema chama chao kimejipanga hivyo ni vyema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wakatenda haki.

“Naiomba NEC itende haki ili ikifika siku ya uchaguzi Septemba 16 upinzani wasipate sababu ya kufanya vurugu,” amesema.

Aidha, Bashe amewataka viongozi wa upinzani kuacha kusema kuwa wanaohamia CCM wamenunuliwa kwani kuna wengi wamehama chama tawala na kwenda upinzani lakini lakini hakuna aliyesema amenunuliwa.

“Kati ya waliowahi kuhama upinzani ni pamoja na Mgombea wa CCM wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara, Mgombea wao wa Monduli, Julius Kalanga na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Naomba wapinzani watuambie waliwapa Sh ngapi hawa?

“Vyama vya siasa ni sawa na gari unapanda likupeleke mahali, ukiona halikufikishi unashuka, ndivyo alivyofanya Waitara,” amesema Bashe.

Amesema kwa sasa CCM ndiyo chama pekee chenye demokrasia ambapo kinaruhusu kukosoana, kuzungumza na Waziri Mkuu yupo, jambo ambalo Chadema hawawezi.

“Huko kwao hakuna hayo mambo, ni zidumu fikra za mwenyekiti kwa hiyo naomba waangalie nyumba yao waache haya mambo ya kusema watu wamenunuliwa,” amesema Bashe.

Kwa upande wake Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, amesema tatizo la upinzani wakipelekewa ulinzi wanasema CCM imewapelekea mashushushu.
“Lengo la hayo maneno yao ni ili hiyo siku wamteke wenyewe huyo dada ahlafu waseme ametekwa,” amesema Lusinde.

Naye Waitara amesema wakati akiwa mbunge kupitia Chadema, mgombea wa sasa wa Chadema alikuwa akimhujumu wakati akitaka kuandaa mikutano ya kuzungumza na wananchi.
“Asia alikuwa akinikwamisha kwa kuwanunulia pombe vijana waliotakiwa kuandaa mikutano ili wasifanye hivyo.
“Wao walikuwa wanaangalia mipango ya mwaka 2020, nimelalamika kwa viongozi wote lakini hakuna hatua iliyochukuliwa, nikaamua kuondoka,” amesema Waitara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles