Gabriel Mushi, Dodoma
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), amesema mfumo wa kodi nchini umesababisha gharama za uzalishaji bidhaa kuongezeka na kudumaza mazingira rafiki ya uwekezaji.
Pia ameitaka Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, kukutana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji yatakayomsaidia Rais John Magufuli kutimiza ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
Bashe ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akichangia mjadala wa bajeti na kuongeza kuwa licha ya mwaka 2016 kumwambia waziri husika, Charles Mwijage kuwa anasubiri aone miujiza katika wizara hiyo, hadi sasa inashangaza kuona hakuna kilichotokea.
“Muujiza wa kwanza ulikuwa ni kuona namna gani Wizara ya Viwanda inaweza kuunganisha mambo matatu ambayo amekabidhiwa. Rais aliamua kwa makusudi kuunganisha biashara, viwanda na uwekezaji ili kufikia lengo la mapinduzi ya viwanda.
“Lakini hadi leo tunazungumzia General Tyre, Liganga na Mchuchuma. Kuna matatizo ya msingi ya biashara lakini huoni kwenye mpango wetu namna ya kuyashughlikia,” amesema.
Amesema licha ya Mwijage kutaja vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19, hakuna mpango unaoonesha kuondoa matatizo yaliyopo kwenye mifumo ya kodi, miongozo na sheria katika kufanya biashara nchini.
“Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia katika mazingira ya kufanya biashara Tanzania nchi ya 137 kati ya nchi 190 kidunia na nchi ya 150 katika kutoa vibali,” amesema Bashe.