Na Imani Nathanieli, Mtanzania Digital
Katibu wa Baraza la Ulamaa(BAKWATA) na Msemaji wa Mufti, Sheikh Hassan Chizenga, amesema kutokana na wimbi la tatu la Uviko-19, kusambaa ulimwenguni ikiwamo Tanzania, baraza hilo limeona umuhimu wa kukutana kujadili suala hilo kwa jamii ya kiislamu, hasa baada ya Serikali kutoa muongozo.
Shekhe Chizenga amesema kuwa ibada ndio jambo la muhimu kuliko yote kwa kuwa ndio kiunganishi kati ya mwanadamu na Mungu, hivyo haina budi kuendelea huku muongozo wa Wizara ya Afya ukizingatiwa.
Ametaja mambo mbalimbali ya kuzingatia wakati wa ibada ni kuwa na vifaa vya kujikinga, waumini kukaa umbali wa mita moja, juhudi za kutakasa mikono ziongezwe na ziwe za kudumu.
Ameeleza kuwa mambo hayo yafanyike kabla na baada ya ibada kwa sababu watu ambao ni rahisi kuambukizwa ni wale wenye afya ambazo si imara.
“BAKWATA inaishukuru Serikali kwa hatua ya kuagiza chanjo za Uviko 19 nchini na kuifanyak uwa ni jambo la hiari ili yeyote anayezihitaji azipate bila kutaabika.
“Hii ni fursa adhimu kwa wale wanaokusudia kutekeleza ibada ya Hijja na Umra siku za usoni,” amesema Chizenga.
Ameongeza kuwa waumini wajiepushe kupeana mikono au kubusu katika kipindi hiki kwa lengo kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo, huku waumini wote nchini wakifanya Dua mbalimbali.
“Dua ndio silaha ya muumini, Allah amesema katika Qurani Saratul Furqaan Aya ya 77,” amesema Chizenga.