25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Baba: Mwacheni Mo apumzike

NA ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAKATI wingu zito likiwa bado limetanda kuhusu kutekwa kwa Mohamed Dewji (Mo), baba yake amesema kwa sasa mfanyabiashara huyo maarufu anahitaji mapumziko zaidi.

Hadi sasa haijajulikana kwa watekaji hao ambao bado hawajanaswa namna walivyomrudisha Mo na hata kufika katika eneo la Gymkhana lililopo mita chache kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi, jambo ambalo linaendelea kuzua mjadala.

Hatua ya Mo kutelekezwa katika eneo hilo linazua maswali kutokana na eneo hilo kuwa karibu na ofisi nyeti za ubalozi, mashirika ya kitaifa na kimataifa, hoteli na majengo makubwa yanayoaminika kuwa na kamera za usalama.

Ujasiri wa watekaji hao kumwachia Mo katika eneo hilo na kisha kulitelekeza gari walilotumia kumteka, likiwa limebadilishwa namba za usajili, ni miongoni mwa mambo yanayozua maswali.

Mwishoni mwa wiki Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro wakati akitoa ripoti ya awali ya uchunguzi kuhusu tukio hilo, alisema watu waliomteka Mo walitumia gari aina ya Toyota Surf lenye namba za usajili AGX 404 MC ambalo alionesha picha zake na zaidi akisisitiza kuwa vijana wake hawatalala kwa kazi ya kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapatikana.

Gari hilo ndilo hilo hilo lililomtelekeza, likiwa limebandikwa kwa gundi namba za usajili T 314 AXX huku kwenye vioo zikibaki namba zile zile za awali.

KAULI YA FAMILIA

Akizungumza na MTANZANIA jana jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya kuachiwa kwa Mo na watu wasiojulikana, baba mzazi wa mfanyabiashara huyo, Gulamhussein Dewji alisema kwa sasa afya yake ni njema, japo anahitaji mapumziko.

Alisema kuwa tangu Mo aliporejea nyumbani alfajiri ya Jumamosi, Oktoba 20 hali yake kiafya haina mashaka na kijana wake anaendelea vizuri, japokuwa amepewa nafasi ya mapumziko nyumbani kwake.

Alisema kwa sasa hana mengi ya kuongea zaidi ya kushukuru ushirikiano ambao anaendelea kuupata kutoka Jeshi la Polisi hata baada ya kupatikana kwa kijana wake.

“Mohammed hajambo, anaendelea vizuri na kwa sasa amepumzika nyumbani. Ninachoweza kusema kwa sasa ni kushukuru tu ushirikiano tunaoendelea kuupata kutoka Polisi,” alisema.

Taarifa zilizotolewa juzi na IGP Sirro zilieleza kuwa Mo aliyetekwa alfajiri ya Alhamisi Oktoba 11 akiwa katika eneo la mazoezi la Hoteli ya Colloseum alipatikana baada ya kutelekezwa katika eneo la viwanja vya Gymkana jijini Dar es Salaam.

Alisema pamoja naye, pia gari iliyotumika kumteka ilitelekezwa katika eneo hilo na watuhumiwa kutokomea kusikojulikana.

MAMBOSASA NA WATUHUMIWA

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema jeshi hilo linaendelea na oparesheni ya kuwasaka watuhumiwa wa utekaji nyara huo hadi watakapopatikana.

Alipoulizwa iwapo kuna yeyote aliyekamatwa miongoni mwa watu waliotelekeza gari linalodaiwa kutumika kumteka Mo kisha kumrejesha na kutelekezwa katika viwanja vya Gymkana, alisema hadi jana mchana hakuna aliyekamatwa.

“Bado tunaendelea na operesheni na hatujawakamata wahusika, ila leo ni Jumapili na tutazungumza kwa kina kesho baada ya kupata taarifa zote zilizokusanywa na watu wetu kwa usahihi,” alisema.

Alisema pia kuwa watu wanane miongoni mwa 27 waliokamatwa tangu kuanza kwa operesheni hiyo kama ilivyotangazwa na IGP, Simon Siro Ijumaa wiki iliyopita bado wanaendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Alieleza pia kushangazwa kwake na taarifa zilizokuwa zikisambazwa mitandaoni jana kuhusu mabadiliko ya ghafla yaliyofanywa katika Jeshi la Polisi na kueleza kuwa amehamishiwa makao makuu katika Kamisheni ya Ushirikishwaji Jamii, akitaka taarifa hizo zipuuzwe kwa kuwa si za kweli.

“Wapuuzeni hao watu, taarifa hizo si za kweli na ninashangaa kwamba watu hao wana nia gani, wanapojaribu kutunga na kusambaza taarifa hizi za uongo, wanatangaza mambo ambayo bado hata hayajawa,” alisema.

NYUMBANI KWA MO

 

Timu ya MTANZANIA ilifika nyumbani kwa Mo jana majira ya saa 9 alasiri ambapo ilielezwa na walinzi wa nyumbani hapo kuwa hawawezi kumwona yeyote kwa muda huo.

Walinzi hao kutoka kampuni ya G1 walisema kutokana na maagizo waliyopewa, hawawezi kuruhusu waandishi wa habari kuingia bila kupata ujumbe wa kutoka kwa wanafamilia waliopo ndani.

Mmoja wa walinzi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake, alieleza kuwa Mo hayupo nyumbani kwake na hata wao hawajamwona, ila wanasikia yuko mapumzikoni.

 

ENEO LA  GYMKANA

Katika eneo la Gymkana walinzi wa viwanja hivyo walisema hawana uhakika kuhusu mtu aliyemfungua kamba za mikono Mo na kumsaidia kupata mawasiliano ya baba yake

Kiongozi wa walinzi hao, Marwa Mseti alisema huenda walikutana na walinzi waliokuwepo usiku lakini hakuna kumbukumbu zozote za mlinzi yupi aliyekutana naye kwanza.

“Sisi pia tumesikia tu kuwa baada ya Mo kutelekezwa katika eneo hili alijikokota na kukutana na walinzi ambao aliwaomba msaada. Ila hatujui ni walinzi gani aliokutana nao, labda uje usiku utakapokutana na waliopo zamu ya usiku wanaweza kujua,” alisema.

Alisema katika hali ya kawaida kwa kuwa Mo alifika mwenyewe katika eneo hilo na kuomba msaada hawakuona kama ni suala linalohitaji kupewa kipaumbele, kwa kuwa waliotekeleza walikuwa katika sehemu ya kutekeleza majukumu yao.

Walisema gari ya watekaji iliyokuwa imetelekezwa kwenye eneo hilo iliondolewa katika eneo hilo juzi, baada ya polisi kumaliza kazi yao ya kuweka kumbukumbu za eneo hilo la tukio na uchunguzi wa awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles