MURUGWA THOMAS -URAMBO
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, imemhukumu kutumikia kifungo cha nje ya gereza miezi sita, Peter Masanja kwa kosa la kumjeruhi mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano kwa sababu ya kukataa kwenda shule.
Masanja alipewa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi wa Wilaya hiyo, Bittony Mwakisu baada ya kufikishwa mbele yake akikabiliwa na shtaka la shambulio la kudhuru mwili.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na mkaguzi wa polisi Joseph Mbwana, ulidai kuwa Masanja alitenda kosa hilo Februari 21, mwaka huu huko Mtaa wa Majengo, Wilaya ya Urambo.
Mbwana aliongeza kuwa siku hiyo, saa 7 mchana, mtuhumiwa alimpiga Adam Peter (5) anayesoma elimu ya awali Shule ya Msingi Ukombozi.
Alidai Masanja alimpiga mtoto na kumjeruhi mgongoni na makalioni kipigo ambacho kilisababisha alazwe hospitali ya wilaya siku mbili kwa matibabu.
Mtuhumiwa alikamatwa na majirani walioshuhudia tukio hilo na kufikishwa polisi.
Mahakama baada ya kusikiliza shauri hilo kwa kina na kuzingatia mazingira na uhusiano, ndipo ikamhukumu kifungo hicho.