Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuweka mpango mkakati wa dharura wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aweso ameyasema hayo leo Januari 23,2024 akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dodoma ambapo alitembelea chuo hicho na chanzo cha maji cha Iyumbu kufuatilia hali ya upatikanaji wa maji chuoni hapo.
Ameihakikishia jumuiya ya chuo hicho na wanachuo kuwa hali ya huduma ya maji itaimarika na kwamba kazi ya serikali ni kuwapatia wananchi wote huduma ya majisafi.
Aweso amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, kuhakikisha anaweka mtandao wa maji unaojitegemea ili kutoa huduma UDOM kutoka chanzo cha maji cha Nzuguni ambapo Wizara ya Maji itawezesha utekelezaji wake.
Aidha, ameitaka DUWASA kuongeza upatikanaji wa maji chuoni hapo kutokana na dharura iliyopo.
Katika hatua nyingine ameagiza kuendelea kufanyika utafiti wa kina katika maeneo ya chuo hicho ili kutambua uwepo wa maji chini ya ardhi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Lughano Kusiluka, amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa majisafi upatao lita 2,296,000 zinazohitajika kuweza kuhudumia wanachuo 33,000.
Kwa sasa chuo hicho kinapata lita 1,172,000 kutoka DUWASA sawa na asilimia 51 kutoka vyanzo vya Mzakwe na Iyumbu.