28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

‘AWAMU YA TANO IMEANZA KUREJESHA MTIZAMO WA NYERERE’

Na THOBIAS ROBERT-MAELEZO


NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, amesema Serikali ya awamu ya tano imeanza kurejea katika mtazamo wa Mwalimu Julius Nyerere juu ya uchumi wa viwanda aliouanzisha.

Akizindua Kongamano la Kumbukizi ya Kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika  Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  jijini Dar es Salaam juzi, Ole Nasha alisema Mwalimu Nyerere alijenga viwanda vingi hapa nchini.

Alivitaja viwanda ambavyo Mwalimu Nyerere alivijenga kuwa ni viwanda vya nguo kama Urafiki, Mbeya Tex, Mwatex, Mutex, viwanda vya ngozi, viwanda vya zana za kilimo, viwanda vya kutengeneza vipuli pamoja na viwanda vinavyotegemea malighafi za mazao yanayolimwa hapa nchini.

Alisema Taifa linahitaji viongozi wazalendo na waadilifu kama alivyo Rais Dk. John Magufuli ambaye ameonesha nia ya dhati ya kufuata nyendo za Mwalimu Nyerere kwa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi yanayotegemea viwanda.

“Serikali ya awamu ya tano kwa muda wa miaka miwili iliyokaa madarakani, imejitahidi kurejea na kuweka kwenye vitendo dhana ya Mwalimu Nyerere ya uchumi wa viwanda, kwani kwa sasa  inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa, mwaka  2016/2017-2020/2021 unayojikita katika ujenzi wa viwanda kama njia ya maendeleo ya kiuchumi na maisha ya watu,”alisema Ole Nasha.

Alisema mtazamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa ni kutumia viwanda vya ndani kama njia ya kujinasua kutoka kwenye unyonyaji wa muda mrefu.

Kama Taifa huru kuna haja ya kuondoa tofauti za kisiasa na kuishi katika misingi ya usawa, umoja, ushirikiano ili kujiletea maendeleo ya uchumi kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, ikiwemo kuhimiza uzalendo kwa kila mtanzania ili kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbumbuku ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila, alisema kuwa ili kufikia Tanzania ya viwanda taifa linahitaji viongozi wazalendo wenye uchu wa maendeleo na wasio na misingi ya ukabila wala udini.

“Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa, ili tuendelee tunahitaji vitu vinne ambavyo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, hivyo ustawi wa uchumi wa viwanda  unahitaji viongozi na watendaji ambao ni wazalendo, watiifu na wenye kutanguliza mbele masilahi ya taifa,”alisema Profesa Mwakalila.

Kongamano la maadhimisho ya siku ya  Mwalimu Nyarere hufanyika kila mwaka ili kujadili busara, fikra na hekima zake katika kujenga usawa, maendeleo, umoja na ustawi wa uchumi wa taifa letu.

Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 18, tangu Mwalimu Nyerere afariki mnamo Oktoba 14, 1999, ambapo kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu inasema “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.

Maadhimisho hayo yatafanyika visiwani Zanzibar ambapo shughuli ya kuzima mwenge wa uhuru itafanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles