25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU ASHAURI VIONGOZI WAOMBEWE WATENDE HAKI

Na JANETH MUSHI

WATANZANIA wametakiwa kuliombea taifa  kuwahimiza   viongozi wa Serikali na vyombo vinavyotoa haki  kwa wakati ikiwamo Mahakama  kuzingatia utoaji wa haki.

Rais Dk.John Magufuli pia ameombwa kuingilia kati suala la  wabunge kukamatwa kamatwa ovyo  na Jeshi la Polisi.  

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Askofu Mstaafu wa Kanisa la TAG, Jimbo la Kilimanjaro, Glorious Shoo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Kanisa  hilo, Timothy Wambura.

Walikuwa  wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kumtembelea Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema),   katika Mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo, Arusha.

Mchungaji Shoo alisema  Tanzania ina sifa nyingi nzuri ila suala la haki na utu limeanza kuleta dosari.

Alisema  ni suala ambalo linahitaji kutupiwa macho kwa sababu  linaweza kuliletea taifa dosari kubwa.

Alisema  wabunge, viongozi na wananchi wanapaswa kutambua kukosekana kwa haki ni tatizo la jamii nzima na kila kiongozi kwa nafasi yake anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba.

"Rais wetu amejitahidi kufanya mambo mengi mazuri ila tunahitaji kutupia macho mfumo wa utoaji wa haki  kwa wakati.

“Taifa lina sifa nyingi ila  jambo linalosikitisha ni suala la haki na utu limeanza kuleta dosari na linaweza kutia doa taifa letu.

“Tunaona mapambano ya rushwa na dawa za kulevya yanavyofanywa ni mazuri ila yafanyike kwa misingi ya haki na sheria,"alisema na kuongeza:

"Mimi si mwanasiasa lakini nahimiza haki kwenye jamii, namsihi Rais aingalie treatment ya wabunge.

“Haki isiposimama katika taifa, taifa huanza kunyong'onyea…kila kiongozi ailinde katiba na wananchi tuungane kuliombea taifa na kusihi wahusika  tuilinde amani ambayo ni tunda la haki".

Alisema   wamefarijika kumtembelea kiongozi huyo na kuwa walikwenda  kumtia moyo, kumfariji na kuomba naye  na kuwa suala kubwa walilozungumza naye ni haki ambayo huliinua taifa.

Naye Mchungaji Wambura alisema   watanzania wanapaswa kuungana na kuwa wamoja hasa katika kusisitiza suala la sheria na utekelezaji wake   haki iweze kuonekana.

"Tunahitajika tuwe na umoja, nimetamani ule umoja wa zamani, nimeona   hatuzungumzi lugha moja.

“Ningetamani uongozi kwa ngazi zote uwawezeshe watanzania waishi kwa raha,  watu wenye dhana kuwa hawatendewi haki waridhishwe ili waione hiyo haki," alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles