Gaudence Msuya -Kibiti
WANAFUNZI 1,708 wa shule za msingi Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, wanatarajia kunufaika na msaada wa chakula na sare zinazotolewa na shirika linalojihusisha na kampeni ya elimu kwa wasichana la Camfed.
Mradi huo ulitambulishwa rasmi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mohamed Mavura na viongozi wa Camfed.
Meneja Miradi wa Camfed, Anna Sawaki, alisema shirika hilo lililoanza shughuli zake wilayani Kibiti mwaka 2017, limeamua kuongezea mradi mwingine wa kuwasaidia wanafunzi yatima na walio katika mazingira magumu .
Alisema kupitia mradi huo, wanafunzi 1,708 walio katika shule 28 za msingi wilayani hapa watanufaika kwa kupewa chakula, sare, madaftari na vifaa vingine vinavyohusiana na elimu.
Sawaki alisema awamu ya kwanza ya mradi huo itakuwa ni kuwajengea uelewa walimu wakuu wa shule 28 na maofisa elimu kata wa kujua namna ya kushiriki ambapo Sh milioni 58 zitatumika wakati wa awamu ya pili.
“Kupitia mradi huu tunatarajia wanafunzi 1,708 yatima na walio katika mazingira magumu watanufaika kwa kupatiwa chakula, sare za shule na vifaa vingine kama vitabu na daftari, lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata elimu,” alisema Latifa Sabuni ambaye ni ofisa mradi wa Camfed mkoani Pwani.
Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mussa Kalanje alisema mradi huo utasaidia wanafunzi ambao wanaishi katika kaya masikini kuhudhuria masomo darasani na kuepuka utoro.
“Idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawahudhurii kwa wakati masomo darasani ni wale yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, kwa mradi huu tunaamini watahudhuria masomo ipasavyo,” alisema Kalanje.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mohamed Mavura aliyaomba mashirika mengine kujitokeza kusaidia sekta ya elimu hasa wasichana ili kuwezesha wanafunzi wa wilaya hiyo kupata elimu ya juu.