LONDON, ENGLAND
KOCHA wa timu ya Arsenal, Mikel Arteta, ameongezewa majukumu mengine ya kuwa meneja wa timu hiyo baada ya kuonesha makubwa kwa kipindi cha miezi tisa.
Arteta alitangazwa kuwa kocha wa timu hiyo Desemba mwaka jana akichukua nafasi ya Unai Emery, lakini kwa kipindi cha miezi tisa tangu achukue timu hiyo ameweza kutwaa mataji mawili ambayo ni Kombe la FA pamoja na Ngao ya Jamii.
Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Vinai Venkatesham, amesema uongozi wa timu hiyo umefanya maamuzi hayo kutokana na kile alichokifanya tangu siku ya kwanza baada ya kutangazwa kuwa kocha mkuu.
“Hakuwa kocha mkuu tangu siku ile anatangazwa, ila tangu hapo ameweza kufanya makubwa zaidi ya kuwa kocha mkuu, tumeutambua mchango wake tangu siku ya kwanza na tunaamini anaweza kuwa mtu mwenye kuleta mabadiliko makubwa ndani ya kikosi chetu.
“Tunaamini nafasi ya ukocha inakuwa kwa ajili ya kuwafundisha wachezaji, lakini kwa uwezo wake anafaa kuwa meneja ambaye anaisimamia timu yote kwa ujumla ikiwa pamoja na safu ya makocha.
“Kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba majukumu yake yatakuwa yanaongezeka na tunaamini atayaweza kwa kushirikiana na viongozi wenzake,” alisema Venkatesham.
Arteta alijiunga na timu hiyo na kupewa jukumu la kuwa kocha mkuu moja kwa moja akitokea Manchester City ambapo alikuwa kama kocha msaidizi chini ya Pep Guardiola.
Akiwa Manchester City alifanikiwa kutwaa mataji mbalimbali kama vile Ligi Kuu England mara mbili mfululizo na mataji mengine, hivyo Arsenal wakaamini kuwa kocha huyo msaidizi anaweza kuwafanyia makubwa akiwa kocha wao mkuu.
Hata hivyo, Arsenal wanaamini chini ya kocha huyo msimu huu wataleta upinzani mkubwa na wanaweza kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi kwa ajili ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.