LONDON, England
KLABU ya Arsenal imegundua mchezo mchafu unaofanywa na Barcelona ambao wanatajwa kumshawishi straika wao, Pierre-Emerick Aubameyang kujiunga na timu hiyo yenye maskani yake Camp Nou.
Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Hispania vinasema, straika huyo raia wa Gabon yupo tayari kujiunga Barcelona ili akaiongoze safu ya ushambuliaji hiyo na Lionel Messi.
Arsenal inaamini Barcelona wanatumia watu wao kumshawishi straika huyo kuondoka Emirates ili kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Hispania, La Liga.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta hataki kumwachia nyota huyo, kwani anamuhitaji katika kujenga timu yake kwa ajili ya msimu ujao, huku mkataba wake ukiisha mwaka 2021 ndani ya klabu hiyo ya London.
Inaelezwa kama msimu huu ukimalizika na Arsenal wakishindwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, mastaa wengi wanaweza kuondoka ndani ya timu hiyo.
“Nawapenda mashabiki wa hapa, tangu nilipokuwa mdogo nilipenda kuwa hapa, nilikuwa naiangalia Arsenal sababu ilikuwa inaundwa na wachezaji wakubwa na kushinda mataji.
“Nafikiri ni jambo zuri kuwa hapa, nina furaha, siwezi kujua hatma yangu lakini kwa kipindi hiki ni vizuri kuwa hapa,” alisema Aubameyang.
Straika huyo aliteuliwa kuwa nahodha wa Arsenal baada ya Granit Xhaka kupokonywa kwa kushindwa kuelewana na mashabiki wa timu hiyo, Novemba mwaka jana.
Aubameyang alimaliza mfungaji bora msimu akiwa na mabao 20 sawa na washambuliaji wawili wa Liverpool, Mohamed Salah na Sadio Mane.
Msimu huu, tayari amefunga mabao 17, akizidiwa mawili na kinara Jamie Vardy katika mbio za kuwa mfungaji bora wa msimu.
Washika Bunduki wapo tayari kuendelea kuwa na straika wao, ndio maana wameanza maongezi ya kumpa mkataba mpya baada ya huu kumalizika mwakani