LONDON, ENGLAND
KIVUMBI cha Ligi Kuu nchini England kiliendelea jana kwa michezo mitatu, huku mchezo wa mapema ukiwakutanisha Arsenal kwenye uwanja wa nyumbani Emirates dhidi ya Brighton na kushinda mabao 2-0.
Arsenal waliutawala mchezo huku wakitumia mfumo wa 3-4-3, wakati huo wapinzani wao wakitumia mfumo wa 4-4-1-1.
Arsenal walianza mchezo wao kwa kasi huku wakitafuta bao la mapema la kuongoza, walifanikiwa kulipata katika dakika ya 16 lililowekwa wavuni na Nacho Monreal kutokana na shambulizi kali walilolifanya.
Hata hivyo, baada ya kupata bao hilo bado walionekana kuliandama lango la wapinzani wao kwa kutafuta bao la pili, lakini walikosa kuzitumia nafasi mbalimbali walizozitengeneza.
Brighton walijaribu kufanya mashambulizi makali katika dakika ya 23, lakini mpira wao uligonga mwamba. Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Arsenal walikuwa wamepata bao moja.
Baada ya kipindi cha pili kuanza, bado wageni walionekana kuwa katika wakati mgumu kutokana na Arsenal kulishambulia lango lao kwa kasi.
Waliweza kuongeza bao la pili katika dakika ya 56, ikiwa ni dakika 11 baada ya kipindi cha pili kuanza, bao hilo liliwekwa wavuni na mshambuliaji wao  Alex Iwobi baada ya kupokea pasi ya kisigino iliopigwa na mshambuliaji wao Alexis Sanchez.
Katika dakika ya 71 kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alifanya mabadiliko kwa kumtoa Iwobi ambaye alipachika bao la pili na nafasi yake kuchukuliwa na Theo Walcott na akatoka Alexandre Lacazette, huku nafasi yake ikichukuliwa na Olivier Giroud.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha mchezo huo katika matokeo, hivyo hadi dakika 90 zinamaliza Arsenal waliondoka uwanjani hapo huku wakiwa na furaha kutokana na matokeo hayo.