AZIZA MASOUD na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
SASA ni dhahiri hatua ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk. Jacob Chimeledya, kumvua wadhifa wa uaskofu Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa umezidi kulipasua kanisa hilo.
Jana viongozi wa lanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, walitoa taarifa kwenye vyombo vya habari wakisisitiza kumtambua Askofu Mokiwa.
Si hilo tu, mapambano ya pande mbili zinazopingana juu ya uamuzi huo, yalionekana waziwazi jana baada ya kuvuja kwa taarifa za Askofu Mokiwa kutaka kufanya mkutano katika Kanisa la Ilala, Dar es Salaam na hivyo kila upande kuita polisi.
VIONGOZI WA DAYOSISI
Taarifa ya viongozi wa Dayosisi ya Dar es Salaam iliyosainiwa na wajumbe wapatao 19, imekanusha habari zilizogaa kwenye vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii, kwamba viongozi hao wamekubaliana na uamuzi wa askofu wao mkuu wa kumwondoa katika nafasi yake Askofu Mokiwa.
Viongozi hao wakiwamo wajumbe wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam, ambao wamesema wanaungwa mkono na mapadre, mashemasi, wainjilisti na walei, walisisitiza kuwa Dayosisi ya Dar es Salaam haina mgogoro kama ilivyozungumzwa na Askofu Mkuu Dk. Chimeledya bali kuna mambo ambayo yamepandikizwa ili kumchafua Dk. Mokiwa.
“Sisi wajumbe wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam, Viongozi wa Dayosisi, tukiungwa mkono na walei ambao ni waumini katika Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, tunapenda kuufahamisha umma kuwa hatuna aina yoyote ya mgogoro au matatizo na Askofu wetu Kanuni Dk. Valentino Mokiwa.
“Ukweli ni kwamba Askofu Mkuu wa Jimbo la Anglikana Tanzania amefanya makosa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kukubali kudanganywa na kundi la watu wachache linaloongozwa na wale walioondolewa kwenye mamlaka za upadri na kutengwa na dayosisi,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kutokana na uwepo wa kundi hilo, Askofu Chimeledya amejikuta akifanya uamuzi wake binafsi bila kuhusisha Nyumba ya Maaskofu na kujikuta akilipaka matope kanisa analoliongoza badala ya kulitetea na kuliweka katika mwelekeo wa kiroho na maendeleo.
Ilikwenda mbali na kueleza kuwa msingi wa matatizo hayo yote ni kikundi cha waasi waliopo katika dayosisi hiyo wasiozidi watu 30 ambao wapo kwa lengo la kulipaka matope kanisa.
“Tunasisitiza kumtambua Dk. Valentino Mokiwa kuwa Askofu Kanuni wa Dayosisi ya Dar es Salaam, tunamuomba awe na uvumilivu na kuwasamehe wote wanaomdhihaki na kumtukana, tunamuombea aendelee kuwa katika huduma yeye pamoja na familia yake.
“Lengo la watu hao ni kutaka kanisa liyumbe, kumbukeni kuwa baada ya barua ya Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania aliyoileta kukataliwa na Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi yetu Januari 7, Askofu Mkuu alipeleka barua hiyo katika kanisa lililoasi Magomeni na kuagiza isambazwe,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa barua hiyo ilisambazwa kinyume na taratibu ambapo katika Kanisa la Magomeni limeundwa kundi la vijana ambalo kazi yao ni kuzunguka katika makanisa ya dayosisi kuusambaza waraka wenye kumdhalilisha Askofu Mokiwa.
Pia taarifa hiyo ilieleza vijana hao kwa sasa wamekuwa wakifanya vurugu katika makanisa na mfano mmoja wapo ni zile zilizotokea katika Kanisa la Ubungo Januari 15.
“Tunawaomba Wakristo wenzetu katika dayosisi msikubali vishawishi, epukeni, kataeni vikundi vyenye kueneza chuki na faraka katika dayosisi yetu, huo si wito wa Mungu, tulieni, msiogope, ombeni kwa msaada wa Mungu tunavuka salama katika dhoruba hili,” ilieleza taarifa hiyo.
ULINZI WA POLISI
Jana Jeshi la Polisi lililazimika kuweka ulinzi katika Kanisa la Mtakatifu Nicholaus lililopo Ilala Dar es Salaam ili kuzuia vurugu ambazo zingeweza kutokea.
Hatua ya polisi kuzingira kanisa hilo saa mbili asubuhi, ilikuja baada ya kuvuja kwa taarifa za Askofu Mokiwa kutaka kulitumia kanisa hilo kufanya mkutano na waumini wanaomuunga mkono.
Dk. Mokiwa licha ya kuvuliwa uaskofu amegoma kuachia ngazi, kwa madai kuwa hana tuhuma zozote zinazomkabili licha ya kamati ya kushughulikia malalamiko dhidi yake kudai kugundua makosa 10, ikiwamo kufuja mali za kanisa na kujinufaisha binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kanisa hilo, Dk. Mokiwa aliomba ulinzi wa Jeshi la Polisi ili afanye mikutano yake na waumini wanaomuunga mkono.
Upande wa pili ambao hamuungi mkono, nao ulifika katika ofisi za Jeshi la Polisi na kuweka zuio la kuomba mkutano huo usifanyike kwani Dk. Mokiwa sio askofu tena.
Taarifa ya mkutano wa Dk. Mokiwa ilisomeka hivi:
YAH: KIKAO/COMMITEE B.
Wajumbe wa Halmashauri ya kudumu kuhudhuria kikao cha S/COMITTEE kitakachofanyika kesho trh 21 Januari baada ya kikao cha bodi ya fedha. Katibu wa Dayosisi. NK. Baba askofu NK.VG. NK wajumbe mgt mnaombwa kuhudhuria.
Huku wa upande wa pili uliojitambulisha kama ni walei wa Mkoa wa Dar es Salaam, ukisomeka hivi;
Waumini wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya DSM, kesho wamejipanga kufanya maandamano makubwa Januari 21, kumzuia Mokiwa kuendelea na kazi za uaskofu na kuzuia kikao cha bodi ya fedha na baadaye halmashauri ya kudumu.
Hima Mwanglika na popote ulipo ukipata ujumbe huu jiandae twende tukalitetee kanisa lako na maandamano yataanzia ulipo na ikifika saa 2 uwe kanisani Mt. Nicholaus Ilala AMEN.
Hata hivyo kikao cha Dk. Mokiwa hakikufanyika tena kama kilivyotangazwa na maandamano yaliyokuwa yamepangwa na walei hayakufanyika.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kuhusu uwepo wa polisi katika kanisa hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alisema hakuna kilichotokea na kwamba ulinzi ni kazi za kawaida za polisi, hivyo hakukuwa na lolote.
MTANZANIA Jumapili pia lilimtafuta kiongozi wa walei, Sylivester Haule kuzungumzia hilo, ambaye alisema ni kweli baada ya kuona tangazo la mkutano wa Dk. Mokiwa na wao wakaenda Polisi Ilala kuweka zuio la mkutano huo.
Alisema waliandika barua kwa RPC Mkoa wa Ilala kuomba zuio la mkutano huo, lakini majira ya saa mbili asubuhi magari ya polisi mawili yalikuwapo katika eneo hilo kwa ulinzi.