26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

ALIZETI INAPUNGUZA UMASIKINI KIPATO

ay-cicegi-tarlalari_903263

Na Joseph Lino,

TANZANIA ni kati ya nchi kumi zinazoongoza katika uzalishaji wa alizeti duniani, kwani alizeti inalimwa maeneo mengi nchini na wakulima wadogo wadogo.

Kuendeleza sekta ya kilimo cha alizeti ambayo inazidi kukua kila mwaka inaweza kuongeza tija katika mchakato wa kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda.

Sekta hii inawahusisha sana wakulima wadogowadogo na hivyo inaweza kuboresha maendeleo ya maisha ya kila siku ya watu wa kipato cha chini.

Kwa maelezo ya Jukwaa Huru la Wadau wa Kilimo (ANSAF), linasema takwimu za mwaka wa 2014/15 zinaonyesha kuwa Tanzania ilizalisha zao la alizeti kiasi cha tani milioni 2.8.

Katibu Mtendaji Mkuu wa ANSAF, Audax Rukonge, anasema uwezo wa kuchakata alizeti inaozalishwa ni tani milioni moja tu huku Tanzania ikiwa inaagiza mafuta ya chakula kwa wingi kutoka nje.

“Uagizaji wa mafuta ya chakula Tanzania hupoteza dola za Marekani milioni 358 kwa mwaka ambayo ni asilimia 2.6 ya dola bilioni 13.6 za fedha zinazotumika kuagiza bidhaa,” anasema Rukonge.

Anaelezea zaidi kuwa kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha kiwango kati kinahitaji Sh milioni 70 ambacho kinaweza kuzalisha tani tano kwa siku na halmashauri nyingi zina uwezo wa kuwekeza kwenye hilo.

“Kwa hali ya Tanzania ikiwemo rasilimali watu, hali ya hewa, maeneo ya mashamba nchi inaweza ikazalisha asilimia 100 kwa mahitaji yote ya ndani na kuuza nje,” anaelezea Rukonge. Mafuta ya alizeti ni bora kwani hayana rehemu.

Katika Ripoti ya Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Alizeti 2016-2020 ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, inasema Tanzania inazalisha asilimia 2.4 ya alizeti yote duniani.

Sekta ya alizeti ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania kwa vile ina uwezo wa kutoa sehemu kubwa ya mafuta ya chakula nchini ambayo kwa sasa sehemu kubwa ya mafuta hayo huagiza kutoka nje.

“Pamoja na ukuaji wa sekta ya alizeti, Tanzania inapaswa kupunguza utegemezi wa kuagiza mafuta ya chakula kutoka nje,” kwa maelezo wa ripoti hiyo.

Hivi sasa zaidi ya nusu ya mafuta ya chakula huagizwa kutoka nje na takwimu za sasa zinaonesha kuwa uzalishaji wa ndani kutoka viwanda vikubwa na vidogo zinachangia asilimia 40 ya ugavi wa mafuta ya chakula nchini.

Kwa ujumla bidhaa zinazotokana na alizeti nchini zimeongezeka mara  sabini zaidi kithamani na hivyo kuleta mapinduzi makubwa katika kuuza nje kutoka dola za Marekani milioni moja hadi kufikia dola milioni 70 katika kipindi cha miaka kumi.

Asilimia 80 ya alizeti ya Tanzania huuzwa nchini India, licha ya soko la dunia kukabiliwa na ukuwaji kwa asilimia 15 katika muongo mmoja uliopita, Tanzania imeweza kufanya vizuri katika soko la dunia kufikia kwa wastani wa  asilimia 50 ya ukuwaji kila mwaka.

Katika kipindi hicho mchango wa Tanzania katika soko la dunia umekua kutoka asilimia 0.04 mwaka 2005  kufikia asilimia 0.24 mwaka 2010 na asilimia 0.49 kufikia 2014.

Ripoti inaelezea kuwa mbali na umuhimu wa sekta hii kwa walaji nchini, pia kuna nafasi nzuri ya kufaidika na soko la nje kutokana na mahitaji makubwa ya alizeti ulimwenguni ambapo Tanzania inaweza kujitosheleza katika mauzo ya ndani na nje ikiwa na mzunguko wa thamani wa alizeti kama mbegu, mafuta na mashudu.

Kwa mkakati wa kuendeleza sekta ya alizeti kuanzia 2016-2020, unatarajia kuchochea soko la mbegu bora kushawishi sekta binafsi kuzizalisha zaidi mbegu aina nne hadi sita ambazo ni mbegu mpya ifikapo 2020.

Aidha, mkakati huu unalenga kusaidia upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima wadogo na kujenga mazingira yatakayowezesha hali hiyo kuwa endelevu.

Lengo jingine la mkakati wa kuongeza thamani na uzalishaji wa alizeti ni kujenga mazingira ya kilimo cha mkataba baina ya wakulima wadogo, wa kati na wazalishaji wa mafuta au wanunuzi wa zao hilo.

Katika kutekeleza hilo mradi utahakikisha kuwapo kwa huduma muhimu kama vile ushauri, taarifa za masoko na huduma za kifedha kwa wakulima.

Pia vyama vya ushirika vya wakulima wa alizeti vitajengewa uwezo wa kujiendesha kushawishi mabadiliko ya sera na kusimamia kilimo cha mkataba kinachopendekezwa.

Uzalishaji wa alizeti ulimwenguni umeongezeka katika kipindi cha miaka 20 iliyopita kutokana na mavuno bora na maeneo ya kulima.

Sehemu kubwa ya alizeti hutumika katika kutengeneza mafuta ya chakula na asilimia tano tu kutumika katika kutengenezea vitafunwa na chakula cha wanyama.

Mafuta ya alizeti dunia nzima mauzo ya nje yanafikia dola za Marekani bilioni 10, takwimu za mwaka 2014 ambayo sawa na tani milioni 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles