27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEDAKA‘UCHAWI’ WA ZAHERA AAHIDI SHANGWE

THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo, baada ya kuwaahidi kuendelea kupata raha bila kuwapo kwa kocha wao mkuu, Mwinyi Zahera.

Mwandila kwa sasa anakaimu nafasi ya kocha mkuu wa timu hiyo, majukumu aliyobeba baada ya Zahera kutimkia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambako ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Florence Ibenge ndiye Kocha Mkuu wa kikosi cha DRC, ambacho kinawania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Misri.

Mwandila chini ya majukumu yao ya sasa, ataiongoza Yanga kuivaa Lipuli FC, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Jumamosi hii Uwanja wa Samora, Iringa.

Miamba hiyo ya Jangwani itakutana na Lipuli, ikiwa na kumbukumbu na kupata ushindi wa mabao 2-1, katika  mchezo uliopita dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwandila, ambaye ni raia wa Zambia, alisema wanafahamu wanakwenda Iringa kukutana wapinzani imara, lakini wamejipanga kupambana kwa nguvu na kuhakikisha wanavuna pointi tatu kama ilivyokuwa kwenye michezo yao ya nyuma.

“Tunatarajia kuondoka kesho (leo) kwenda Iringa tukiwa kamili kwa ajili ya mchezo huo, nafahamu Lipuli ni timu nzuri, kwani hata tulipokutana nao mzunguko wa kwanza hatukupata ushindi kirahisi.

“Hata hivyo tutatumia mapungufu yao kupata ushindi na kuendeleza rekodi ya ushindi,” alisema.

Alisema wachezaji wake wapo katika hali nzuri kimwili na kiakili kuelekea mchezo wao huo wa keshokutwa.

“Wachezaji wote ambao wapo kwenye programu watasafiri, isipokuwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ambaye amefungiwa mechi tatu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“Tumefanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa nyuma, ili yasijirudie kwa mara nyingine na kutuvurugia mkakati wetu wa kupata pointi tatu,” alisema.

Timu hizo zilipokutana katika  mchezo wa mzunguko wa kwanza  dimba la Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli.

Yanga inashika usukani kwenye  msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kujikusanyia pointi 67, kati ya mechi 27 ilizocheza, ikishinda michezo 21, sare nne na kupoteza miwili.

Wapinzani wao, Lipuli FC wanashika nafasi ya tano, wakijikusanyia pointi 41, kati ya mechi 29 walizocheza, sawa na KMC iliyojikita nafasi ya nne, ikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles