Na Esther Mnyika,Mtanzania Digital
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kuna haja kwa Afrika kuharakisha uwekaji wa mazingira bora ya kuwezesha ushiriki thabiti wa wanawake katika biashara ili kuweza kuzalisha ajira nyingi nakufikia maendeleo endelevu.
Akizungumza leo Desemba 8,2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya ufungaji wa kongamano la pili la wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuchukua hatua ili kuwa na mabadiliko ya haraka ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara.
“Ni imani yangu kwamba katika siku tatu za majadiliano katika kongamano hili kila mmoja ameongeza uzoefu na uelewa wa namna ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika biashara ndani ya eneo Huru la biashara Barani Afrika”amesema.
Amesema ili kukabiliana na changamoto zilizobainishwa nchi zote za Afrika hazina budi kuwa na dhamira ya dhati ya kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika majadiliano .
Ameeleza kuwa kukiwa na nia thabiti ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa ,kutatoa hamasa kwa nchi rafiki na washirika wa maendeleo kwa kushirikiana na Bara la Afrika ili kufikia lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia ushiriki wao katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika.
“Ni matumaini yangu kwamba maazimio ya kongamano hili yatakuwa chachu ya kuandaa na kutekeleza ajenda ya Dk.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinara wa uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika”amesema.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wanawake na Watoto wa Zanzibar, Riziki Pembe Juma aliwahamasisha wanawake wafanya biashara kuendelea kuongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na utafutaji wa soko la bidhaa wanazozalisha ndani na nje ya bara la Afrika.
Kongamano la pili la wanawake katika biashara ndani ya eneo huru la biashara barani Afrika limewakutanisha wadau wa sekta ya biashara kutoka nchi 55 za bara la Afrika.