Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Chama cha Alliance for Democrating Change (ADC ), kimetoa rai kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuchukua hatua kwa vyama ambavyo vitashindwa kufuata katiba yake.
Akizungumza na MTANZANIA DIGITAL Julai 20, 2023 Mwenyekiti wa ADC, Hamad Rashid amesema katiba zote za vyama vya siasa zimevitaka vyama kulinda tunu za Taifa ikiwemo amani na upedo.
“Hakuna katiba ya chama chochote cha siasa nchini ambayo haisemi kuhusu ulinzi wa tunu za Taifa letu lakini vyama vinavunja katiba zao,” amesema Rashid.
Amesema demokrasia inahitaji ulinzi wa amani nchini hivyo vyama kama taasisi vinapaswa kusimamia haki.
Akizungumzia kuhusu 4R yaani Reconciliation, Resilience Reform na Rebuilding amesema vyuo vikuu vinapaswa kutengeneza mifumo itakayoshughukia uchunguzi pindi 4R zitakaposhindwa kusimamiwa ndani ya taasisi(vyama).
“Hizi 4R azitafanya kazi kama rushwa haitakoma ofisi ya msajili inapaswa kuchukua hatua za haraka pindi sheria zitakapovunjwa bila kuangalia chama kiwe kikubwa au kidogo,” ameeleza.
Naye, Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo amesema kutokana na ukuaji wa Teknolojia nchini ameitaka ofisi ya msajili kuingia kwenye mfumo wa digital ili kuwapunguzia vyama vya siasa uhifadhi wa nyaraka muhimu za ofisi zao.
Amesema kwasasa nchi imeingia kwenye mfumo wa Tehama lakini ofisi ya Msajili bado imekuwa ikitumia mfumo wa zamani wa kukusanya nyaraka .
“Rai yangu ni kwa ofisi ya msajili itoke kwenye mfumo wa analogia ihamie digital itupunguzie mrundikano wa makaratasi kwenye ofisi zetu,” amesema Doyo.
Amesema kuwa pamoja na kuingia kwenye mfumo wa digital Serikali inapaswa kuimarisha miundombinu ili kuepuka changamoto ambazo zimekua zikijitokeza mara kwa mara kwenye mifumo ya digital.
“Tulikuwa tunahangaika na mfumo wa BRELA ambao tunapaswa tutumie kujisajili mpaka naongea na wewe tuna siku ya pili hatujafanikiwa mtandao unakata tu, Serikali inapaswa kuimarisha hii miundombinu.
Doyo ameipongeza Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu shughuli za siasa kuendelea katika maeneo mbalimbali nchini Kwani hii inatoa fursa ya ukomavu wa demokrasia nchini.
Amesema ADC itaendelea kufanya siasa za kistaarabu bila kuvunja Sheria za nchi.