26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

ACT Wazalendo yakata rufaa NEC

NA LEONARD MANG’OHA -DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kimeamua kuwasilisha rufaa za wagombea wake walioenguliwa katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) bila kupitia kwa wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya, kwa madai kuwa hakina imani nao.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban, alidai kuwa iwapo watawaachia wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya wapeleke nakala hizo za rufaa na wakaona utetezi ambao awali wao waliamua kuudharau, wataweza kunyofoa baadhi ya nyaraka na kuwasilisha ambazo hazijakamilika.

Pia alisema kuwa wameamua kupeleka tume ili wakati itakapopokea nakala za wasimamizi wa uchaguzi ilinganishe na zile zilizowasilishwa na chama hicho.

“Baada ya wagombea wetu kuwekewa mapingamizi na hatimaye kuenguliwa, tumewaambia wakate rufaa. Sasa kwenye hii hatua ya rufaa kilichotokea wapo ambao walipewa fomu namba 12 kwa ajili ya rufaa na wapo ambao hawakupewa fomu namba 12.

“Hao tumewaambia waandike barua moja kwa moja tume kupeleka malalamiko ya kunyimwa fomu ya rufaa ambayo ni haki yao kimsingi, lakini wapo ambao walikata rufaa.

“Sasa tuna rufaa zaidi ya 50 za wagombea wetu ambazo kwa mujibu wa kanuni zinataka tuzipeleke kwa wasimamizi wa uchaguzi ambao wao kama ‘transit’ ziende Tume ya Uchaguzi kutolewa uamuzi.

“Kwa sababu ya imani yetu ndogo sasa kwa wasimamizi wa uchaguzi wilaya, chama kiliwataka wagombea wote walete nakala zao za rufaa makao makuu na chama kimechukua hatua ya kuziwasilisha kwa Tume ya Uchaguzi.

“Kwa barua hii mnayoiona hapa, tumewasiliana na Tume na Uchaguzi na tumewaeleza kwanini tumepeleka sisi, na tumewaeleza kwenye barua yetu kwamba pamoja na kutambua kwamba wasimamizi wa uchaguzi ndio wenye jukumu la kuwasilisha fomu na nyaraka nyingine za rufaa kwa Tume ya Uchaguzi, chama chetu kimekuwa na imani ndogo na wasimamizi hao wa uchaguzi hususan walivyoshughulikia pingamizi dhidi ya wagombea wetu.

“Hivyo tumeona ni vema kuleta taarifa za wagombea wetu za uwepo wa rufaa ili kuepusha hujuma yoyote dhidi ya nyaraka za rufaa tulizoziwasilisha wakati tukisubiri tume kuwaita wagombea wetu kuwasikiliza wakati ambapo tume itaona inafaa,” alisema Shaaban.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimelalamikia namna ambavyo mapingamizi waliyowekewa wagombea wake wa nafasi za udiwani na ubunge yalivyoshughulikiwa, ikiwamo kuenguliwa kwa sababu zisizo za msingi kama kutoandika kirefu cha jina la chama hicho jambo ambalo alisema si kosa kwa sababu kupitia katiba ya chama hicho kama kilivyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kinatambuliwa kwa jina kamili ama ufupisho wake.

Shaaban alisema kuwa chama hicho hakipingi wagombea wake kuwekewa pingamizi kwa kuwa ni suala la kikanuni, lakini wanachohoji ni namna ambavyo mapingamizi yalivyoshughulikiwa.

Alizitaja baadhi ya sababu nyingine zilizotumiwa na wasimamizi wa uchaguzi kuwaondoa wagombea wao kuwa ni pamoja na baadhi ya wagombea kuwa watumishi wa umma, kutotimiza idadi ya wadhamini pamoja na makosa mengine ambayo aliyataja kuwa ni madogo ambayo hayastahili kumwondoa mgombea kama vile kutotumia alama za mkato na kituo.

Shaaban alisema chama chao kinapinga baadhi ya wagombea wao kudaiwa kushtakiwa, kuwekewa pingamizi hewa, kutolewa uamuzi bila kupewa nafasi ya kusikilizwa na baadhi kupewa barua za uamuzi kabla ya pingamizi.

Aliiomba NEC kutenda haki na baada ya kuwarudisha wagombea hao walioenguliwa iwaondoe wasimamizi wote waliohusika au iwabadilishie vituo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles