Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Akiba (ACB), Silvest Arumasi amesema wataendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahitaji ya huduma za kibenki.
Akizungumza wakati wa hafla iliyohusisha viongozi na watumishi kutoka wizara, taasisi na ofisi mbalimbali za Serikali jijini Dodoma amesema Akiba Commercial Bank Plc imekuwa mstari wa mbele katika kujenga mahusiano na wadau wake wakiwemo wateja, mamlaka, taasisi pamoja na Serikali.
Amesema hafla hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya wadau wa benki hiyo ikiwa ni sehemu ya kujenga mahusiano mazuri na imara na vyombo mbalimbali.
Amesema benki pia imeonyesha ari na azma ya kuangalia wananchi wa Dodoma kwa upekee kutokana na ongezeko la mahitaji ya kibenki kufuatia fursa mpya zinazojitokeza jijini humo.
Amepongeza juhudi za Serikali katika kuendeleza na kustawisha makao makuu Dodoma na kuahidi kuwa benki itaendelea kuiunga mkono kwa kuboresha huduma na kupanua wigo kuwafikia wananchi wengi zaidi na hatimaye kutimiza azma ya kutoa mchango mkubwa wa huduma shirikishi za kifedha yaani Finacial Inclusion.
Amesema benki itaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahitaji ya huduma za kibenki.
“Tunaomba washiriki mtoe maoni, mirejesho kwa lengo la kuboresha huduma za benki yetu, tunategemea mengi kutoka kwenu,” amesema Arumasi.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kufahamiana, kuweka mikakati ya pamoja ya jinsi ya kuwahudumia watumishi wa umma kwa weledi zaidi na kutatua kero zinazojitokeza katika utendaji.