25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaoagiza magari Japan watahadharishwa

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

UBALOZI wa Tanzania uliopo nchini Japan, umetoa ushauri wa kuzingatiwa kwa Watanzania wanaoagiza magari. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi, Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Emmanuel Buhohela, ubalozi huo umekuwa ukipokea malalamiko mengi kutoka kwa Watanzania wanaodhulumiwa fedha wakati wakijaribu kununua magari nchini humo kwa njia ya mtandao. 

“Malalamiko hayo pia yanahusisha kutotumiwa magari yao kwa wakati na kutumiwa magari ambayo hayana sifa na vigezo vilivyoainishwa kwenye mtandao.

“Ubalozi kwa nyakati tofauti umefuatilia kwa karibu suala hili na kwenye mamlaka husika za Japan, na unatoa ushauri ili kuepuka matatizo hayo yasijitokeze tena,” alisema Buhohela.

Aliwataka Watanzania wanaoagiza magari nchini humo kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutuma fedha kwa mtu ama kampuni inayojihusisha na uuzaji wa magari.

“Kabla ya kuagiza gari, ni vyema kuangalia tovuti zaidi ya moja ili uweze kulinganisha bei na kufahamu bei ya wastani ya gari husika. 

“Kampuni inayouza gari kwa bei ya chini sana kuliko nyingine lazima itiliwe shaka. Inashauriwa utume barua pepe kwa taasisi iliyosajiliwa na kutambulika na Serikali ya Japan (Japan Used Motor Vehicle Exporters Association – Jumvea) ili wakusaidie kufanya uhakiki wa kampuni husika,” alisema Buhohela.

Alisema kuwa kwa wanaoagiza magari wanaweza kuhakiki kampuni yoyote hata kama si mwanachama wao na kwamba huduma hiyo hutolewa bure.

“Ukiwa na shaka nunua gari kampuni ambayo ni mwanachama wa Jumvea, kuna kampuni zaidi ya 250 ambazo ni mwanachama wa Jumvea na wanatumia mfumo maalumu wa malipo – Jumvea Safe Trade (Just) ambao unamlinda mteja,” alisema Buhohela.

Alisema kwa maelezo zaidi mteja anaweza kutembelea tovuti ya https://jumvea.or.jp ama kutumia kampuni za kijapani zenye matawi nchini na kutambulika kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

“Ikumbukwe kuwa fedha ikishatumwa Japan ni vigumu sana kurejeshwa kutokana na sheria za nchi hiyo. Mamlaka za kisheria za Japan kama polisi na waendesha mashtaka huanzisha shauri dhidi ya kampuni au mtu aliyekiuka mkataba, hupokea mikataba halali inayotambulika Japan kama ankara za malipo ambazo huwa nazo.

“Ubalozi unawasihi watu wote kuzingatia ushauri uliotolewa na kufuata taratibu za biashara za kimataifa ili waepuke kutapeliwa au kudhulumiwa,” alisema Buhohela.

Alisisitiza kuwa kutuma fedha za kigeni bila kupata mali tarajiwa si tu kunaleta madhara makubwa kwa mtumaji na familia yake, bali huharibu akiba ya nchi ya fedha za kigeni bila kupata thamani tarajiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles