Na Walter Mguluchuma-Katavi
WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ameonekana kushangazwa na Mkoa wa Katavi kusifika kwa imani za kishirikina, licha ya kuwa miongoni mwa mikoa ya mwanzo kabisa kuingia kwa dini ya Romani Katoliki miaka 135 Iliyopita.
Alisema sifa hiyo ni mbaya na inatia aibu mno.
Pinda aliyasema hayo jana, wakati wa ibada ya kusimikwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Eusebius Nzigilwa.
Alisema mkoa huo, pamoja na dini kuingia mapema bado umeendelea kuwa na sifa ya kuwa na uchawi, jambo ambalo sasa halipo, hivyo watu wasiwe na hofu ya kuutembelea.
Alisema ushirikina sio sifa nzuri kabisa, unaharibu sifa ya mkoa huu ambao bado ni mpya, lakini umekuwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi.
Alisema kanisa limekuwa na mchango mkubwa wa kuleta maendeleo ya nchi na limetoa mchango wa kuinua elimu na kuboresha afya ya Wanzania ambao wamekuwa wakipata huduma za afya kwenye vituo vyake.
Alisema Serikali inathamini michango ambayo imekuwa ikitolewa na viongozi wa dini, hivyo wanaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa madhehebu yote ya dini bila kufanya ubaguzi wowote ule .
Alisema rais amefikisha taifa kwenye uchumi wa kati kuna kazi kubwa imefanyika.
Aliwataka Watanzania wamtie moyo Rais Dk. John Magufuli ili taifa lizidi kuendelea,kuna baadhi ya mataifa yameanza kuona wivu mafanikio yanayoendelea kupatikana.
Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Askofu Gerevansi Nyaisonga alisema kanisa hilo litaendelea kushilikiana na Serikali kuendeleza amani ya nchi ili amani iliyopo izidi kuendelea na nchi zidi kuwa na amani zaidi .
Aliomba ushirikiano ulipo sasa na madhehebu ya diniuzidi kuendelea na wao wataendelea kuhubiri amani.
Askofu Nzigilwa alisema amekwenda Jimbo la Mpanda kuwa mtumishi na wala sio mtumikiwa.
Jimbo hilo lina waamini 231,000 kati ya wakazi 825,880 ya wakazi wa Mkoa wa Katavi kwa mujibu ya sensa ya mwaka jana.
Askofu Nzigilwa aliwekwa wakfu wa kuwa Askofu msaidisi wa Jimbo kuu la Dares Salaam Machi 19, 2010.