30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

KWISHA KAZI! Simba yaibomoa Yanga, yaipa Namungo tiketi ya Shirikisho Afrika

 ZAINAB IDDY -DAR ES SALAAM 

TIMU ya Simba imeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga, katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho(FA), maarufu Kombe la Azam, uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 

Simba sasa itaumana na Namungo katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo utakaochezwa Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga. 

Hata hivyo, ingawa Simba ndiyo iliyopata ushindi mnono hapo jana, kicheko kisichoelezeka kitakuwa kwa Namungo ambayo imehakikishia tiketi ya kuiwakilisha Tanzania, katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao. Namungo ilianza kukata tiketi ya fainali ya michuano hiyo, baada ya kuilaza bao 1-0, timu ya Daraja la Kwanza ya Sahare All Star ya Tanga. 

Iko hivi, kulingana na kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania, bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara hupata fursa ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati yule wa Kombe la Azam hukata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 

Lakini ikitokea bingwa wa Ligi Kuu na yule wa Kombe la Azam ni yule yule, timu iliyomaliza nafasi ya pili Kombe la Azam ndiyo hupata fursa ya kuiwakilisha Tanzania Kombe la Shirikisho Afrika. 

Hii ina maana kwamba, hata kama Namungo itapoteza mchezo wa fainali dhidi ya Simba, tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika itasalia kwenye mikono yake, kwakua tayari Simba ina ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika. 

Mabao ya Simba jana yalifungwa na Gerson Fraga dakika ya 21 , Clatous Chama dakika ya 49, Luis Miquissone dakika ya 51 kabla ya Mzamiru Yassin kupiga la nne dakika ya 89. 

Bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Feisal Salum dakika ya 69. 

Mchezo ulianza kwa Yanga kutawala na kupeleka mashambulizi ya kasi langoni mwa Simba. 

Lakini kadri dakika zilivyokuwa zinasonga Simba ilionekana kuwamudu wapinzani wao. 

Dakika ya nne, kipa wa Yanga, Metacha Mnata alipangua mkwaju wa Luis.

Dakika ya 21, Fraga aliipa uongozi Simba kwa kuifungia bao la kuongoza akiunganisha pasi makini ya Chama. 

 Baada ya bao hilo, Simba ilioonekana kuongeza presha kwenye lango la Yanga. 

Dakika ya 31, mkwaju wa John Bocco ulitoka nje kidogo ya lango la Yanga, baada ya kupokeza pasi ya Chama. 

Dakika ya 37, mwamuzi Ramadhan Kayoko alimlima kadi ya njano beki wa Yanga, Lamine Moro kwakumkwatua 

 Luis kabla ya Juma Abdul kulimwa kadi ya njano dakika ya 44 kwakumkwatua Francis Kahata wa Simba. 

Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0. 

Kipindi cha pili, Simba ilionekana kudhamiria kuibuka na ushindi mkubwa kwani ilizindua mashambulizi mapya langoni mwa Yanga. 

Dakika ya 49, Chama alipokea pasi makini ya Bocco na kuiandikia Simba bao la pili kabla ya Luis kufunga la tatu dakika ya 50 baada ya kuwazidi kasi mabeki wa Yanga. 

Dakika ya 58, pasi ya Nchimbi aliyeingia kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima ilimfikia Benard Morrison lakini kipa wa Simba, Aishi Manula aliwahi kutokea na kuuweka kwenye himaya yake. 

Dakika ya 58, Mohamed Hussein alilimwa kadi ya njano baada ya kumkwatua Abdul. 

Wakati huu, Yanga ilionekana kupata nguvu zaidi na kulisakama lango la Simba. 

Dakika ya 64, mpira wa kichwa uliopigwa na David Molinga ulipaa juu kidogo ya lango la Simba. 

Dakika ya 65, Feisal alilimwa kadi ya njano baada ya kumkwatua Luis. 

Dakika ya 69, mpira wa kichwa uliopigwa na Patrick Sibomana ulimfikia Feisal ambaye aliujaza mpira wavuni kwa shuti kali na kuipa Yanga bao la kwanza. 

Bao hilo lilifufua matumaini ya Wanayanga kwa kiasi fulani, ikionekana kama inaweza kuyagomboa mabao ya wapinzani wao. 

Lakini ule usemi wa ‘ng’ombe wa masikini hazai ulionekana kuing’ang’ania Yanga kwani ilijikuta ikifungwa bao la nne dakika ya 89, lililofungwa Mzamiru, baada ya Simba kufanya shambulio la kushtukiza. 

Dakika 90 za mwamuzi Kayoko zilikamilika kwa Simba kutakata kwa mabao 4-1 dhidi ya wapinzani wao Yanga. 

Kikosi Simba: Aishi Manula, Mohammed Hussein, Kenndy Juma, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Luis Miquissone/ Miraji Athumani dakika ya 88,Gerson Fraga/ Muzamiru Yassin dakika ya 80,John Bocco/ Meddie Kagere dakika ya 72, Clatous Chama na Francis Kahata/ Hassan Dilunga (dk) 72. 

Kikosi Yanga: Metacha Mnata,Juma Abdul,Jafar Mohammed,Lamine Moro,Said Makapu,Papay Tashishimbi/ Kelvin Yondan dak ya 54, Feisal Salum Abdallah, Haruna Niyonzima/ Ditram Nchimbi dak 54, Deus Kaseke,David Molinga na Bernard Morrison/Patrick Sibomana dakika ya 68. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles