Oliver Oswald Na Ruth Mnkeni, Dar es Salaam
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema yupo tayari kufungwa jela kuliko kuendelea kuwavumilia watu wanaokwamisha ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kukimbilia mahakamani.
Sambamba na hilo, pia amepiga marufuku uchimbaji wa mchanga pembezoni mwa mto uliokuwa eneo la daraja la Lugalo, ikiwa ni pamoja na kuwapa tahadhari ya kuwafungia wafanyabiashara walio karibu na eneo hilo endapo watashindwa kuwa walinzi wa uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Hayo aliyasemwa jijini Dar es Salaam jana, katika ziara yake ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara pamoja na madaraja unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Alisema Serikali imekuwa ikisikitishwa na vitendo vya uharibu wa miundombinu hiyo vinavyofanywa na baadhi ya watu, licha ya serikali kutumia gharama kubwa katika ujenzi wa miundombinu hiyo.
“Watanzania wanapaswa kujifunza na kuacha ubinafsi katika shughuli za maendeleo ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa katika kiwango kinachostahili, kwa kuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa miundombinu ya barabara.
“Kwa kiasi kikubwa uharibifu wa miundombinu umechangia kuwepo kwa ucheleweshaji wa kukamilika kwa baadhi ya miundombinu, kwani hadi sasa milingoti saba ya taa za barabarani pamoja na mifuniko ya maji taka 12 imeshaibiwa,” alisema Dk. Magufuli.
Kutokana na hali hiyo, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, kuhakikisha anasimamia na kudhibiti vitendo hivyo kwa kuwachukulia sheria wahusika.
Alisema Serikali hadi sasa imeshatumia Sh trilioni moja katika kukamilisha ujenzi wa miradi saba, ambayo ni pamoja na mradi wa barabara za Mwenge-Tegeta uliogharimu Sh bilioni 89, Morocco Sh bil 288, barabara ya chini Tazara Sh bilioni 1.2 pamoja na fly over Sh bilioni 100.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa daraja la Kigamboni lililogharimu Sh bilioni 214, ambapo ujenzi wa madaraja mawili ya Lugalo pamoja na Mlalakuwa lenye uwezo wa kubeba tani 180, yamekamilika na yameanza kutumika.
Alisema pia jumla ya Sh bilioni mbili zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa taa zitakazotumika katika barabara hizo, ambapo fedha zote zimetokana na ufadhili wa serikali ya Japan.
Akizungumza katika ziara hiyo, Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, alisema serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa shughuli za kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa miundombinu hiyo.
“Tunatarajia ujenzi wa mradi wa barabara ya juu (fly over) Tazara kukamilika ifikapo Oktoba au Novemba pamoja na daraja kutoka Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere hadi mjini,” alisema Okada.
Mungu akubariki hata uwe rais 2015-2020