MWANDISHI WETU
WAISLAMU kote duniani wamesherehekea Sikukuu ya Eid ul-Fitr huku wengi wakiwa chini ya vizuizu vilivyowekwa na mataifa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona.
Sikukuu ya Eid moja ya sherehe muhimu kwenye kalenda ya Uislamu huashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramdhan na huadhimishwa kwa ibada ya swala, dhifa za chakula na manunuzi ya zawadi pamoja na mavazi.
Hata hivyo mwaka huu sherehe za Eid zinaandamwa na kiwingu cha janga la corona huku nchi nyingi duniani zimetangaza kurejesha vizuizi ambavyo kwa sehemu vililegezwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Katika hali ya kupunguza msisimko wa sherehe hizo mataifa kadhaa ikiwemo Saudi Arabia, Uturuki, Misri na Syria yamepiga marufuku ibada za umati, moja ya tukio muhimu katika sikukuu ya Eid, kwa lengo la kuzuia kusambaa virusi vya corona.
Nchini Saudi Arabia, yaliko maeneo mawili tukufu kwa dini ya Uislamu, serikali ilitangaza kuwa swala ya Eid itafanyika kwenye misikiti mikuu ya Makka na Madina bila kuhudhuriwa na waumini.
Msikiti mkuu mjini Makka hautembelewi na waumini tangu mwezi Machi na ukimya umegubika eneo la Kaaba – tufe kubwa jeusi ambalo waumini wote wa Kiislamu hufanya ibada kwa kuzingatia mwelekeo wa mahali lilipo.
Saudi Arabia imeanza marufuku kali ya kutotembea nje itakayodumu kwa muda wa siku tano baada ya maambukizi ya Covid-19 kuongezeka zaidi ya mara tatu na kufikia visa 68,000 tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Msikiti wa Al-Aqsa uliopo mjini Jerusalem, ambao ni wa tatu kwa utukufu ndani ya uislamu utafunguliwa tena kwa waumini kuutumia baada ya sikukuu ya Eid.
Nchini Lebanon, taifa lenye idadi kubwa ya waislamu wa madhehebu ya Sunni Serikali imetangaza kufunguliwa kwa misikiti kwa ibada ya swala ya Ijumaa pekee. Lakini waumini watalazimika kupimwa joto la mwili na kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya virusi vya corona.
Wakati huo huo Waislamu barani Asia kuanzia Indonesia, Pakistan, Malaysia hadi Afghanistan walifurika kwenye masoko kwa maandalizi ya sikukuu ya Eid na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa masharti yaliyowekwa kupambana na virusi vya corona. Katika baadhi ya wakati polisi ilijaribu kutawanya makundi makubwa ya watu.
“Kwa zaidi ya miezi miwili watoto wangu wamesalia nyumbani. Sikukuu hii ni kwa ajili ya watoto na ikiwa hawatoweza kusherehekea wakiwa na vitu vipya, haitokuwa na maana ya sisi kufanya kazi kwa bidii mwaka mzima” alisema Ishrat Jahan, mama wa watoto wanne akiwa katikati ya soko la mji wa Rawalpindi nchini Pakistan.
Huko Indonesia, taifa lenye idadi kubwa ya waislamu duniani, watu wanajaribu kuwatumia walanguzi na nyaraka bandia za kusafiria ili kukwepa marufuku zilizowekwa mwishoni mwa mwezi wa Ramadhan, mwenendo unaotishia kuongeza maambukizi.