30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Ngoma nzito wabunge 15 Chadema

 RAMADHAN HASSAN Na FARAJA MASINDE -DODOMA/DAR

WAKATI jana wabunge 15 wa Chadema waliojiweka karantini wakihitimisha siku 14 walizojipa ili kujitenga kama njia ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, baadhi yao walifika na kuingia bungeni na zaidi waliendelea na vikao vya Bunge licha ya Spika Job Ndugai kueleza kuwa hakuna yeyote aliyetekeleza masharti yaliyotolewa.

Aidha kulikuwapo na taarifa zinazodai kuwa baadhi ya wabunge hao pia walizuiwa kuingia ndani ya bunge na walinzi lakini pia wengine wakiwa hawajaonekana kabisa.

Wabunge walioonekana ndani ya bunge wakiendelea na vikao ni Frank Mwakajoka (Tunduma), Ester Matiko ( Bunda mjini) na Salome Makamba (viti maalum), huku mbunge Aida Khenan akionekana katika viwanja vya bunge.

Pamoja na baadhi yao kuingia bungeni hata hivyo Spika Ndugai alizuia hotuba ya kambi rasmi ya upinzani kusomwa kwa kile alichosema kwamba kuna masharti ambayo alikuwa ameyatoa na hayajatekelezwa na wabunge hao.

Umuzi huo wa wabunge wa Chadema kurejea bungeni umekuja ikiwa ni siku mbili tu zimepita tangu Ofisi ya Bunge itoe taarifa ya utoro wa wabunge wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Mei 13, mwaka huu jijini Dodoma ilisomeka;

“Ofisi ya Bunge inatoa taarifa kwamba katika siku za hivi karibuni baadhi ya Wabunge wa Chadema wamekuwa watoro kwa kutohudhuria vikao vya Bunge bila ruhusa ya Spika kwa muda wa wiki mbili kinyume na masharti ya Kanuni ya 146 inayosisitiza wajibu wa kila Mbunge kuhudhuria vikao vya Bunge. 

“Aidha, tunapenda ifahamike kwamba Wabunge hao walisusia vikao vya Bunge huku wakiwa wamelipwa posho ya kujikimu ya kuanzia Mei 1 hadi 17, 2020. Kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 5 ya Kanuni za Bunge, Spika alitoa masharti mawili kwa Wabunge hao.

“Kuwataka Wabunge hao kurejea Bungeni au kurudisha fedha walizolipwa mara moja, kwa kuwa haijulikani Wabunge hao walipo, watalazimika kuwasilisha ushahidi kwamba wamepimwa na hawana maambukizi ya Virusi vya Covid-19 kabla ya kuruhusiwa kuingia Bungeni,” ilieleza taarifa hiyo ya ofisi ya Bunge.

Aidha taarifa hiyo iliwataja wabunge hao kuwa ni Freeman Mbowe, Ester Bulaya, Halima Mdee, John Heche, Joseph Mbilinyi na Peter Msigwa.

Wengine ni Rhoda Kunchela, Pascal Haonga, Catherine Ruge, Devotha Minja, Joyce Mukya, Aida Khenan, Upendo Peneza, Grace Kiwelu na Joseph Haule. 

“Hivyo basi, kwa taarifa hii, na kwa mujibu we Kanuni ya 144 ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayohusu usalama katika maeneo ya Bunge, Spika ameagiza Kitengo cha Usalama cha Bunge kutowaruhusu wabunge waliotajwa hapo juukuingia katika maeneo ya bunge kuanzia Jumatano Mei 13, mpaka watakapotimiza masharti tajwa hapo juu,” ilieleza taarifa hiyo ya bunge.

YALIYOJIRI BUNGENI JANA

Akizungumza mara baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya bajeti,Mashimba Ndaki kumaliza kusoma maoni ya Kamati hiyo,Spika Ndugai alisema hawezi kuruhusu hotuba ya kambi rasmi ya upinzani isomwe kwa kuwa kuna masharti ambayo alikuwa ameyatoa na hayajatekelezwa.

Jana Bunge lilikuwa likijadili bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2020-2021 ambapo kwa upande wa upinzani hotuba hiyo inaelezwa ilikuwa isomwe na Jesca Kishoa kwa niaba ya Halima Mdee.

Spika Ndugai alisema hawezi kumruhusu Msemaji Mkuu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni katika Wizara ya Fedha na Mipango, Halima Mdee asome maoni ya kamati hiyo kutokana na kuwa miongoni wa wabunge waliojifukuza wenyewe.

“Mtaona kwamba hotuba ya upinzani hatujaikubali leo na sababu zake zipo wazi za kuikataa hotuba hiyo mwandishi wa hotuba hiyo Mheshimiwa Halima Mdee ni katika watu waliojifukuza wenyewe hapa bungeni kwamba wao roho zao ni muhimu sana kuliko wengine wote na siyekuwepo na lake halipo” alisema Ndugai.

Alisema hawezi kukubali mambo yapitie dirishani wakati wahusika hawajulikani wako wapi.

“Kwa kuwa kuna masharti ambayo Spika alikuwa ameishayatoa ili waweze kurudi na kuanza kushiriki shughuli za Bunge mashariti hayo hayajatekelezwa.

“Haiwezekani kupitishia dirishani kazi zako zikafanyika wakati wewe ulipo hakujulikani kwahiyo tunaendelea na shughuli,”alisema Spika Ndugai.

ATAKA MBUNGE ATHIBITISHE MKONO KULIPWA POSHO

Jana jioni wakati akiahirisha kikao cha Bunge, Ndugai pia alimtaka Mbunge wa Viti Maalum, Rhoda Kuchela (Chadema) kumuomba radhi au kutoa uthibitisho kwamba Mbunge wa Musoma vijijini Nimrod Mkono (CCM) amelipwa posho ya ya kujikimu na Bunge.

Inadaiwa kwamba katika mitandao ya kijamii,mbunge Kunchela alindika kwamba Bunge limemlipa posho ya kujikimu Mkono ilihali hajahudhuria vikao vya Bunge.

“Mfano Kunchela (Rhoda) amemtuhumu Mkono (Nimrod) amelipwa fedha za kujikimu tabia za namna hii nimezikemea Kunchela yule ni baba yake.

“Mkono hamjamuona hapa hata mara moja hakuwepo hapa na anaumwa sana ni mtu wa kuombewa pale alipo hajitambui. 

“Mimi nasema hajawahi kulipwa, tabia hii ya kuropokaropoka na kutamka chochote sio nzuri. Niwaombe tuendelee kumuombea kwani haya yanaichafua familia yake,” alisema. 

 TAARIFA YA CHADEMA

Awali jana Chadema kilitoa taarifa yake kikisema kuwa wabunge wake wote ambao wamehitimisha siku 14 za kujitenga kwa kukaa nyumbani na kutohudhuria shughuli za Bunge, vikiwemo vikao vya Bunge, ndani ya ukumbi na kamati zake katika maeneo mengine ya mhimili huo wamerejea bungeni.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa wabunge hao walitarajiwa kurejea bungeni jijini Dodoma kuendelea na majukumu yao, baada ya kuwa na uhakika kuwa hawana maambukizi ya Ugonjwa wa COVID19. 

Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika alisema Wabunge wa Chadema waliotekeleza uamuzi wa makubaliano ya chama hicho na wabunge, ya kujitenga kwa kutofika maeneo yote ya Bunge, walitekeleza masharti na ushauri unaotolewa na wataalam wa masuala ya afya kuhusu namna bora ya kujikinga au kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

“Kwasasa, kuanzia leo(jana), watarejea bungeni kuendelea na shughuli za kuwawakilisha wananchi, huku wakiendelea kuzingatia tahadhari zote za kujikinga wao na kuwakinga wengine wakiwemo wabunge wengine, Watumishi wa Bunge na wananchi wetu,” alisema Mnyika kupitia taarifa hiyo.

Mei 1, mwaka huu wabunge wa Chadema walianza kutekeleza makubaliano hayo, baada ya kuwepo kwa taarifa za maambukizi ya Ugonjwa wa COVID19 katika maeneo ya Bunge, hususan miongoni mwa Wabunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles