25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bukoba haina shule ya kidato cha tano, sita

Na Nyemo Malecela

HALMASHAURI ya Bukoba mkoani Kagera inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa shule ya sekondari ya kidato cha tano na sita.

Kufuatia changamoto hiyo, Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limezichagua shule za sekondari za Rubale na Nyamahoro ziweze kutoa elimu ya kidato cha tano na sita.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo ambaye alishiriki kikao cha baraza hilo, alisema kufikia Julai shule hizo zinatakiwa kuanza kutoa elimu ya sekondari ya kidato cha tano na sita. 

“Changamoto inayoikumba Halmashauri ya Bukoba ni kwamba shule zake zote za sekondari za kata zinaishia kidato cha nne.

Haya ni maelekezo, tutumie muda tulionao tufanye kila njia ili shule hizi mbili zilizochaguliwa kufikia Julai zianze kutumika,” alisema Kinawilo.

Alisema shule kongwe za sekondari za Nyakato, Kahororo, Rugambwa na Ihungo hizo zipo tangu zamani na zinasimamiwa na Serikali kuu, hivyo Halmashauri zinatakiwa kujenga shule nyingine inazozisimamia yenyewe.

“Kwa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tunayo shule moja tu ya sekondari ya Kagemu ambayo inatoa elimu ya kidato cha tano na sita wakati Bukoba DC hakuna shule yoyote.

“Ndio maana tumeambiwa kufikia Julai Shule ya Sekondari Rubale na Nyamahoro ziwe tayari tumeziandaa kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita,” alisema Kinawilo.

Aliwataka madiwani kuanzia sasa kuweka nguvu katika shule hizo ili zifikie viwango na wataalamu waje kuzikagua na Julai mwaka huu zianze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano.

“Kutokuwa na shule zenye kidato cha tano na sita katika halmashauri kunasababisha ‘gepu’ maana wanaomaliza kidato cha nne wanaotakiwa kwenda kidato cha tano ni wengi, lakini kwa sababu hatuna shule zinazotoa elimu hiyo hawachukuliwi.

“Maana nafasi za wanafunzi zinakuwa chache hata kama mwanafunzi ana alama nzuri bado anabaki kwa kuwa hana shule ya kwenda,” alieleza Kinawilo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bukoba, Solomon Kimilike, alisema halmashauri hiyo ina kata 29 na kila kata ina shule ya sekondari ambayo inaishia kidato cha nne.

“Kutokana na watoto wetu wengi kukosa nafasi ya kusoma kidato cha tano, madiwani wote wameungana kuhakikisha shule za Rubale na Nyamahoro zinakuwa na kidato cha tano na sita ili tuweze kuongeza idadi ya wanafunzi watakaopata elimu ya sekondari ya juu,” alisema Kimilike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles