Christopher Msekena
MUZIKI hauna huruma kabisa kwa wale wanaoufanya kwa njia sahihi. Hicho ndio nakiona kwasasa ninapotazama tasnia hii inayopita kwenye mchakato kuelekea hatima yake njema.
Ukijifanya wewe ni mzee wa kufuata itifaki na usiruhusu udambwi udambwi utawale muziki wako basi uwe na uhakika kwamba, hutachukua raundi nyingi, jina na ngoma zako zitafutwa kwenye orodha ya wasanii wakali.
Siyo kwamba hakuna watu wanaopenda muziki mzuri, haina maana kwamba mashabiki makini wanaopenda kazi ya msanii bila matukio anayoyafanya nje ya sanaa hawapo, wapo tena wengi tu ila wamezidiwa nguvu kizazi cha sasa chenye baadhi ya watu wanaopenda mambo mepesi mepesi.
Wanapenda mtelezo, wanazimika na maisha binafsi ya mastaa badala ya kupenda kazi ya msanii na kushiriki katika kumjenga na kumkosoa na staa ampendae pale anapozingua. Aina hiyo ya mashabiki hawana nguvu tena miaka hii.
Leo tuna utitiri wa kurasa za udaku huko Instagram zenye nguvu za kuendesha vichwa vya wasanii na menejimenti zao. Msanii yupo radhi kuifurahisha mitandao kuliko mashabiki halisi wa muziki wake.
Tuna aina ya wasanii ambao hawana noma kabisa kutengeneza matukio yanayoumiza watu ili wao wapate nafasi ya kuzungumziwa mtandaoni. Rejea tukio la yule mwimba Singeli aliyekufa kifo bandia kule Tanga na kuzua taharuki miongoni mwetu.
Nakukumbusha tu kwamba siku chache baada ya kudanganya kifo, mwimba singeli huyo akaachia ngoma na Lavalava ambayo kwasasa inakimbiza huko YouTube huku akijizolea mashabiki wapya aliowapata kwenye tukio lake la kifo bandia.
Sasa wewe mwenzangu na mimi unayefuata itifaki usitegemee uta-trend kirahisi mbele ya msanii kama huyu mwenye mashabiki lukuki wa toleo hili.
Ingawa wapo wakali kibao wazee wa itifaki wanaofanya muziki wao bila promo zenye ukakasi kwaajili ya mashabiki na wafuasi wao.
Ila ndiyo hivyo mitandao ya kijamii na wengi wanaopenda mambo mepesi mepesi wanawapa nafasi na ushirikiano wa kutosha wasanii wanaotumia promo zenye ukakasi kutafuta nafasi ya kupenyeza muziki wao.