25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mukoba rais mpya Tucta

Gratian Mukoba, rais mpya wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Gratian Mukoba, rais mpya wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, amewabwaga ameshinda nafasi ya rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Mukoba alipata kura 172 huku mpinzani wake wa karibu, Mbaraka Igangula, akipata kura 110 na Peter Omollo alipata kura 68 wakati mwanahabari Dismas Lyasa aliambulia kura tano.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulitawaliwa na mizengwe  miongoni wa wajumbe wa mkutano huo baada ya jina la aliyekuwa rais wa shirikisho hilo, Omary Ayoub kukatwa.

Ayoub alikuwa akiwania nafasi hiyo kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Fedha na Huduma za Ushauri (TUICO), ambako baadhi ya wajumbe waliopinga hatua hiyo walibatizwa jina la UKAWA.

Sintofahamu hiyo ilimlazimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholaus Mgaya, atoe ufafanuzi akisema kuwa   kikao cha Baraza Kuu kilijadili kwa kina suala la   Omary Ayoub kwa mujibu wa Katiba.

Alisema   kikao hicho kiliiangalia  Katiba ibara 16.6.8 ya mwaka 2009 na kubaini kuwa Kamati ya Utekelezaji ya Shirikisho (KUT) ilikuwa sahihi kumsimamisha uongozi rais huyo wa zamani TUCTA.

“Baraza Kuu lilibaini na kukubaliana kuwa ni kweli Ayoub alistaafu kazi kwa mujibu wa barua ya Machi mosi, mwaka jana kutoka TUICO kwenda TUCTA na baada ya kustaafu Tanzania Fertilizer Company aliajiriwa katika Kampuni ya Nuru Enterprises Ltd kuanzia Machi,” alisema Mgaya.

Alisema hatua ya kustaafu kwake ilikuwa ni miongoni mwa  sababu za kiongozi huyo kupoteza sifa kwa mujibu wa sheria za   kuongoza TUCTA.

Mgaya alisema rais huyo wa zamani aliendelea kuwa kiongozi wa TUICO na kama angeendelea kuongoza uamuzi wowote  ambao angeutoa ungekuwa ni batili kwa mujibu wa sheria.

“Baraza Kuu liliamua kuwa hata kama ndugu Ayoub alipata ajira nyingine baada ya kustaafu hakuwa na haki kisheria kuongoza shirikisho bila ya uchaguzi mwingine kufanyika,” alisema Mgaya.

Akizungumza na MTANZANIA  baada ya kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa TUCTA, Gratian Mukoba, aliahidi kufanyakazi ya kuwaunganisha wafanyakazi wote nchini  kupitia vyama vyote vya wafanyakazi nchini.

“Jamani imani huzaa imani, naahidi kushirikiana na ninyi   kulifanya shirikisho letu lizidi kuwa imara zaidi, niwashukuru wajumbe wote kwa kuonyesha imani kwangu nami sitawaangusha,” alisema Mukoba huku akishangiliwa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles