NA DEBORA SANJA, DODOMA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema chama hicho kinatakiwa kuwa karibu na wafanyakazi na kutetea masilahi yao.
Kinana alitoa kauli hiyo mjini hapa jana katika hafla ya kukabidhiwa kadi ya uanachama kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Hotelini, Majumbani, Huduma za Jamii na Ushauri (CHODAWU) iliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Makao Makuu.
Alisema mara nyingi wafanyakazi wamekuwa wakijitetea wenyewe, na kwamba baada ya kukabidhiwa kadi hiyo yeye binafsi atakuwa karibu na CHODAWU.
“CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, lakini chama kimekuwa hakipo karibu sana na wafanyakazi badala yake kimekuwa karibu na Serikali.
“Nadhani chama kina wajibu wa kuwa karibu na wafanyakazi kuangalia masilahi yao, haki, mazingira na kuwasemea,” alisema Kinana.
Alisema tangu alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, amekuwa karibu na Chama cha Walimu (CWT) kwa sababu wameshawahi kumuandikia barua kumwalika katika vikao vingi.
“Ni wajibu wa CCM sasa kama watendaji kuwa wanachama wa chama cha wafanyakazi kupitia sehemu inayowahusu, na miezi michache ijayo nitaanzisha tawi la chama kwa wafanyakazi wa CCM Makao Makuu.
“Dhamira yangu ni kumfanya kila mtumishi wa chama kuridhia kwa hiyari yake kuwa mwanachama wa CHODAWU, nina hakika watapenda kwa kuwa watapata mahali pa kusemea malalamiko yao,” alisema.
Alisema anajivunia kuwa mwanachama wa CHODAWU kwa kuwa hajawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha wafanyakazi.
Kinana pia alimpongeza Rais mpya wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Gratian Mkoba na kuahidi kutoa ushirikiano.