32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi, wafanyabiashara kizimbani kwa udanganyifu

Kulwa Mzee -Dar es salaam

OFISA wa Polisi kutoka Chuo cha Polisi Moshi – CCP, Emmanuel Lameck (44), mtaalamu wa IT na wafanyabiashara wawili, wamefikishwa mahakamani kwa kulisababishia Jeshi la Polisi hasara ya Sh milioni 798.78.

Wamedaiwa kujipatia fedha hizo kwa udanganyifu, wakidai walifunga mifumo ya utambuzi wa watuhumiwa waliokamatwa na wanaoshikiliwa katika vituo vya polisi nane wakati wakijua si kweli, walifunga katika vituo vinne.

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mbele ya Hàkimu Mkazi, Salum Ally.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Donald Mhaiki (39) ambaye ni mtaalamu wa IT na wafanyabiashara, Abdi Ally (48) na Mohyadin Hussein (56).

Wankyo alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kati ya Machi 19 mwaka 2013 na Oktoba 18 mwaka huo, jijini Dar es Salaam walilisababishia Jeshi la Polisi hasara ya Sh 798,789,272.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu kutoka katika jeshi hilo baada ya kujifanya wameweka mfumo wa utambuzi wa watuhumiwa katika vituo nane vya polisi na kutoa hati kwamba mfumo umewekwa wakati wakijua mfumo huo uliwekwa kwenye vituo vinne na si nane.

Wankyo alidai shtaka la mwisho la kutakatisha fedha linawakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa katika pindi hicho walitakatisha kiasi hicho cha fedha huku wakijua zilitokana na zao la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Upelelezi haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Januari 20 kwa kutajwa.

Walirudishwa rumande sababu mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles