NA HUMPHREY SHAO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limewataka walimu wanaofundisha shule za msingi za Serikali kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya umeme kwa wanafunzi.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Meneja wa Afya na Usalama Kazini wa TANESCO, Mhandisi Mayige Mabula, alipokuwa akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Ubungo National Housing.
Alisema ikiwa elimu itatolewa kwa wanafunzi, ni wazi itasaidia kuepuka madhara pindi nyaya za umeme zinapokatika.
“Tunatoa wito kwa walimu nchini kutoa somo la matumizi na madhara ya umeme kwa wanafunzi ili tuweze kupunguza matatizo madogo madogo yanayowakumba watoto katika nyaya za umeme,” alisema Mabula.
Alisema mpango wa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi, una lengo la kuandaa kizazi ambacho kitakuwa kinafahamu vyema matumizi sahihi ya umeme na namna ya kutoa taarifa kwa shirika pindi madhara yanapotokea.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lydia Savela, aliishukuru TANESCO kwa mpango huo na kusema utasaidia namna bora ya kuelewa umeme na matumizi yake.