FARAJA MASINDE
TANZANIA imesheherekea miaka 58 tangu ilipojipatia Uhuru wake mwaka 1961.
Nasema bila kumun’gunya maneno kwamba sherehe hizo zilizofanyika juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza zimefanyika kwa kiwango cha juu.
Hata hivyo, kivutio zaidi kwenye shamrashamra hizo ilikuwa ni kuhudhuria kwa mara ya kwanza kwa Chama Kikuu cha upinzani hapa chini, Chadema, ambayo imetafsriwa kama mwanzo mwingine mpya wa siasa za Tanzania.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa kwa mara kadhaa chama hicho kimekuwa kikisusia sherehe hizo tangu mwaka 2015 ulipofanyika uchaguzi mkuu, ikiwa ni kielelezo cha kutokuunga mkono matokeo yaliyomweka mdarakani Rais Dk. John Magufuli.
Ushiriki wa vyama vingine vya upinzani kama Chama Cha Wananchi (CUF), Chama cha DP, Kushiriki kwa Chadema kwenye sherehe hizi, kunatuma ujumbe mpya kuhusu siasa za Tanzania hasa wakati ambapo hamasa ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 ikiwa ni hoja inayonyanyuliwa na kujadiliwa na kila chama.
Chadema, ambacho kimekuwa kikizisusia sherehe hizi inajumuika na viongozi wa serikali na wale wa chama tawala cha CCM katika wakati ambapo vigogo wakuu waliojiunga na chama hicho wakati wa vuguvugu la uchaguzi uliopita wakiwa wamejiondoa na wengine wakirejea kwenye chama chao kilichowakuza CCM.
Ingawa hatua hii ya Chadema kushiriki kwa mara ya kwanza tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu uliopita imewavutia wengi, wakidadisi sababu zilizopo nyuma ya pazia hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa huenda chama hicho kinaanza kuweka mguu sawa kuelekea uchaguzi mkuu.
Hoja hiyo inapata mashiko na kauli ya chama hicho kinachosema kwamba hakioni sababu ya kuendelea kujiweka kando na sherehe hizo kwa vile kinajiandaa kushika dola katika uchaguzi ujao.
Mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje ya Chadema, John Mrema, anasema suala la chama hicho kuamua kushiriki sherehe za mwaka huu ni tafsiri inayoakisi mwelekeo mpya wa chama hicho kuelekea siasa za usoni.
Kauli ya Mbowe
Awali akihutubia katika sherehe hizo za Uhuru, Rais Magufuli, aliwaita viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na wastaafu kutoa salamu zao.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, alisema Rais Magufuli anayo dhamana ya kuhakikisha si tu demokrasia inalindwa na kukuzwa, bali pia kunakuwapo haki na usawa kwa wote bila kujali tofauti zao.
Anasema: “Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa kuwapo maridhiano, upendo na mshikamano wa Watanzania. Siku ya leo (juzi) ifungue milango ya kupendana, kuvumiliana na kuheshimiana.
“Rais unayo nafasi ya kipekee kuweka historia ya kuweka maridhiano kwani wapo wanaolalamika kuumia, tunaomba uweke utangamano.
“Nimeshiriki maadhimisho haya kuthibitisha misingi ya umoja, mshikamano na undugu miongoni mwa Watanzania.
“Nakuomba Mheshimiwa Rais kutumia nafasi na dhamana yako kulinda demokrasia. Kusiwe na wanaofurahi huku wengine wakilalamika,” alisema Mbowe.
Uamuzi huo wa Chadema kushiriki sherehe hizo za Uhuru imetafsiriwa na wasomi kama namna ya kusaka mbinu mpya kwa chama hicho baada ya ile ya awali ya kususa kushindwa kuwa na tija.
Wasomi wanena
Profesa Gaudence Mpangala, ni Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Kikatoriki Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, ambaye anasema kuwa uamuzi huo unaonyesha ukomavu wa kisiasa dhidi yao.
“Tukio hilo la Chadema kushiriki kwenye sherehe hizo limekuwa ni jambo la busara linaloashirikia kuwa chama hicho na viongozi wake kimekomaa kisiasa kwani kimetambua dhahiri kuwa ni chama chenye watu na uhuru huo unaosheherekewa ni wa watu wenyewe.
“Kwani wewe kama chama cha sisa hauwezi kususia kila kitu, lakini hata kwa serikali yenyewe ni jambo la kupongezwa kama ambavyo Chadema ilikuwa ikilalamika kwani awali Rais alikuwa akisema kuwa kufanya sherehe ni gharama badala yake tulikuwa tukiazimisha kwa kufanya usafi, kwa madai kwamba zilikuwa zikileta gharama zisizo za lazima.
“Hivyo kwa hatua hiyo inaonyesha kuwa ni kuleta elimu kwa wananchi kujua na kuenzi historia yao hivyo, kwa Chadema ni jambo la kupongezwa kwa uamuzi huu wa kushiriki kwenye mambo ya kitaifa,” anasema Profesa Mpangala.
Maoni hayo ya Profesa Mpangala hayapishani na yale ya Dk. Richard Mbunda, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, anayesema kuwa uamuzi huo wa Mbowe unalenga kusaka Demokrasia kwa namna nyingine baada ya mbinu za awali kushindwa kuleta matunda.
“Mfano, ukiangalia katika uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, Chadema na vyama vingine vya siasa vilisusia uchaguzi huo kwakile kilichoelezwa kuwa uwanja wa ushindani haukuwa sawa na badala yake CCM ilibebwa.
“Hivyo, kwa mtazamo wangu, kitendo cha kususia halafu chama kingine kikaendelea tu kama hakuna kilichotokea bila ya kuwapo kwa waraka wowote kuhusu maridhiano na njia nyingine, ndiyo imekuwa msukumo kwa Chadema kusaka njia mpya ya maridhiano kwa kushiriki sherehe za Uhuru ambao Zitto Kabwe anasema haupo, lengo lao likiwa ni kuwashinikiza CCM kukubali ajenda ya kufanya maridhiano ya kuendesha siasa hapa nchini,” anasema.
Dk. Mbunda anasema kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini, ikizingatiwa kuwa Chadema hakijabanwa tu kwenye siasa bali hata kwenye mikutano, kimekuwa kikibanwa mara kwa mara pia kwa kuzuia shughuli za kisiasa nchini.
“Kauli hii ya Chadema ni mbinu ya kuitaka CCM kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kufikia mwafaka baada ya kubanwa kwa muda mrefu, lakini pia lengo jingine ni kutaka kutambulika kama chama cha kisiasa chenye uhalali wa kuendesha shughuli zake nchini kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa kwa maana ya kulinda amani, hivyo huenda mkakati wao huo ukafanikiwa.
“Japo bado hakuna dalili za moja kwa moja za maridhiano kutoka CCM, mtazamo huo unaweza kuwapa nafasi ya wao kupumua kidogo baada ya misukosuko ya muda mrefu,” anasema Dk. Mbunda.
Mbali na Chadema kutoa neno kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda alizungumza kwa lugha ya Kisukuma ambapo muda wote alikuwa akimsifu Rais Magufuli.
John Cheyo
Mwenyekiti wa Chama cha DP, John Cheyo, aliwapongeza Watanzania kwa sherehe za miaka 58 ya Uhuru.
“Mimi nilisherehekea Uhuru nikiwa na miaka 15, nilicheza dansi usiku kucha, sasa leo ni miaka 58, hongereni Watanzania wote,” anasema Cheyo.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alianza na ombi la uwapo wa demokrasia.
Akitumia salamu ya chama chake ya ‘haki’, Profesa Lipumba anasema pamoja na hatua kubwa ya maendeleo inayopigwa, ni jukumu na wajibu wa Rais Magufuli na Serikali kuendeleza misingi ya demokrasia.
ACT yajiweka kando
Wakati Chadema kikijumuika na viongozi wengine wa CCM kwenye maadhimisho hayo, chama kingine cha upinzani ACT-Wazalendo kimesusia sherehe hizo kwa madai kuwa hakioni sababu ya kushiriki wakati hakuna uhuru wa maoni, demokrasia kuzidi kubanwa na vyama vya upinzani kuendelea kuandamwa na dola.
Ofisa Habari wa chama hicho, Suphian Juma, anasema kuwa hizo ni baadhi ya sababu za msingi zinazokifanya chama hicho kususia sherehe hizo.
Kauli ya Rais Magufuli
Rais Magufuli anasema sherehe zimefanyika jijini humo ili kuondokana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea.
“Ikumbukwe hatukufanya sherehe hizi kwa miaka miwili, mwaka 2015 na mwaka 2018, badala yake fedha zake zilifanya kazi za maendeleo. Ndiyo maana tukaamua tufanye sherehe hizi mkoani Mwanza, tofauti na ilivyozoeleka… hii ni kwa sababu ya kubadili mazoea,” anasema Rais Magufuli.
Harakati za Uhuru
Rais Magufuli anasema uhuru ulikuwa ni hatua za mwanzo za harakati za kutaka kulijenga taifa letu.
“Si lelemama, ila ni kazi ngumu ambayo tumevuka milima na mabonde, inatupa fursa ya kufanya tathmini kuhusu wapi tumefikia, katika ujenzi wa taifa letu.
“Na katika hilo, napenda kutumia fursa hii kuzipongeza awamu zote zilizotangulia za uongozi wa nchi yetu kwa kazi kubwa ilizofanya za kuijenga nchi yetu, sio siri katika kipindi cha miaka 58 ya uhuru nchi yetu imepata mafanikio makubwa.
“Na kusema ukweli, kila awamu imefanikiwa kufanikisha haya kuanzia awamu ya kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, awamu ya pili ya Mzee Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi), awamu ya tatu mzee Mkapa (Benjamin Mkapa) pamoja na awamu ya nne ya mzee Kikwete (Jakaya Kikwete).
“Baadhi ya mafanikio tuliyoyapata ni kujenga na kudumisha amani katika nchi yetu. Tangu tumepata uhuru mwaka 1961, nchi yetu imekuwa kwenye amani na hivyo kuifanya isifike sio tu barani Afrika, bali duniani kote kwa ujumla.
Ujenzi wa uchumi
Rais Magufuli anasema sasa kazi iliyopo ni kujenga uchumi wa nchi, kwani Serikali imeamua kusimamia sekta ya viwanda ambapo ndani ya miaka minne viwanda 4,000 vimejengwa.
Anasema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara na reli ya kisasa.
“Hivi majuzi, Shirika la Reli limeanza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi kwa kina Mbowe na nimeona wanafurahia ‘aikambee’. Pia tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya bandari.
“Kwa upande wa umeme mbali ya kutumia gesi asili na vyanzo vingine, tumeanza na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, tunaendelea na mradi wa kupeleka umeme vijijini (REA), ambako kwa sasa idadi ya vijiji vilivyoongezewa umeme vimeongezeka na hiyo ni kuhakikisha tunafanikiwa katika kuimairisha ujenzi wa viwanda,” alisema Rais Magufuli.