Mwandishi Wetu, Mwanza
Serikali imelifungia Kanisa la Mfalme Zumaridi linalomilikiwa na Dayana Bundala (Mfalme Zumaridi) lililopo eneo la Iseni jijini Mwanza kutokana na kuendesha huduma zake kinyume cha sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Dk. Philis Nyimbi amesema kanisa hilo linaendesha ibada kinyume na sheria na katiba ya nchi huku likidaiwa kutumia usajili wa kanisa jingine la Pentekoste Christian Church of Tanzania (PCCT) ambapo amemtaka msajili wa vyama vya kijamii kuchunguza kanisa hilo.
“Kamati na wajumbe wake na vyombo mbalimbali vya dola imejiridhisha pasipo shaka kupitia njia mbalimbali kuona kwamba kanisa hili limekuwa likifanya kazi nje kabisa ya utaratibu kwa mantiki hiyo imeweza kuleta athari kwa watu wengine na Watanzania wengine hivyo tunasitisha shughuli zote zinazoendelea katika kanisa hili hapa.
“Kwa maslahi serikali yetu, shughuli hizo zinasitishwa hapa kanisani lakini na mpaka nyumbani tusione shughuli hizo zikiendelea.
“Kiongozi wa kanisa hili mfalme Zumaridi yeye kwa jinsia ni mwanamke lakini sambamba na hilo amekuwa akijiita mfalme wakati yeye ni mfalme lakini pia na ameendelea kupotosha umma kujiita yeye ni Mungu wa dunia,” amesema.