TURIN, ITALIA
NYOTA wa timu ya Juventus, Cristiano Ronaldo, anaweza kuingia kwenye hatari ya kufungiwa soka kwa miaka miwili kutokana na kitendo chake cha kuondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika.
Mwishoni mwa wiki iliopita mchezaji huyo alikuwa kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya AC Milan, huku Juventus wakifanikiwa kushinda bao 1-0, lakini Ronaldo alitolewa katika dakika ya 55 na nafasi yake ikachukuliwa na Paul Dybala ambaye alikwenda kufunga bao hilo.
Ronaldo alionekana kuchukizwa na kitendo cha kutolewa ikiwa ni mara ya pili ndani ya wiki moja, hivyo mchezaji huyo imeripotiwa kwamba aliamua kuondoka moja kwa moja uwanjani hapo huku zikiwa zimebaki dakika tatu mchezo huo kumalizika.
Kwa mujibu wa mshambuliaji wa zamani wa Italia, Antonio Cassano, amedai mchezaji huyo kama aliondoka uwanjani hapo bila ya sababu za msingi basi atakuwa hatarini kufungiwa miaka miwili kutokana na uvunjaji wa sheria za soka hilo la Italia kuondoka uwanjani kabla ya muda bila ya sababu za msingi.
Vituo vya uchambuzi wa michezo nchini Italia, Sky Sport Italia na Football Italia, viliweka wazi kuwa Ronaldo mwenye umri wa miaka 34, aliondoka uwanjani hapo kabla ya mchezo huo kumalizika.
Cassano mwenye umri wa miaka 37, amekuwa na uzoefu wa soka la Italia na sheria zake, yaliwahi kumkuta hayo wakati anakipiga katika klabu ya AS Roma baada ya kuamua kuondoka kwenye uwanja wa Stadio Olimpico katika mchezo dhidi ya Lazio, lakini alilazimishwa kurudi kabla ya kuondoka kwa kuhofia kukutwa na kifungo hicho.
“Ni kweli aliondoka kabla ya mchezo kumalizika? Mchezaji hatakiwi kufanya hivyo kutokana na sheria za soka la Italia, nilitakiwa kufungiwa miaka miwili kwa kitendo kama alichofanya Ronaldo, lakini nilirudishwa mapema kabla sijaondoka, hivyo kama Ronaldo aliondoka bila sababu za msingi anaweza kukutwa na kifungo hicho,” alisema Cassano.