Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilitishia kumkamata Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare baada ya kutokuwapo mahakamani hapo.
Kauli ya Hakimu Thomas Simba imetolewa baada ya Mdhamini wa mshtakiwa, Paschal Mwita kudai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo hakuwapo mahakamani na kwamba amesafiri kwenye shughuli zake za ubunge.
Wakili Mwandamizi wa serikali, Pamela Shinyambala alidai kuwa barua ya ruhusa ya mshtakiwa huyo ambaye hivi sasa ni Mbunge wa Bukoba Mjini, ameiona leo (jana) na kwamba upelelezi haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine.
Hata hivyo, Hakimu Simba alionya kuwa ubunge wake (Lwakatare) usiwe sababu ya kuahirisha kesi hiyo na alipanga kuisikiliza tena Desemba 21 mwaka huu.
Katika kesi hiyo, Lwakatare na Joseph Ludovick wanadaiwa kuwa Desemba 28, 2013 katika eneo la King’ongo, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walikula njama za kujaribu kumdhuru aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky kwa njia ya sumu.
Kwa sasa Msacky ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la MTANZANIA.