HADIJA OMARY, LINDI
Serikali imewahakikishia vijana 18,800 wanaotekeleza mradi wa ulimaji wa bustani Kibiashara kupitia teknolojia ya kitalu nyumba kuwatafutia masoko ya uhakika ya bidhaa zao ili kilimo hicho kiweze kuwa na muendelezo.
Mradi wa ulimaji wa bustani kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba pamoja na ujenzi wa vitalu nyumba unatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu kupitia Programu ya Taifa ya kukuza Uchumi ambayo inaendeshwa katika Halmashauri 83 nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Atony Mavunde baada ya kutembelea na kukagua vitalu Nyumba vilivyojengwa na Vijana wa kijiji cha Mwananyamala Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea na kitalu cha vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani humo kilichopo Mtaa wa Ngongo Tulieni.
Mavunde amesema Lengo kuu la mradi huo ni kutoa mafunzo yatakayo wawezesha Vijana kupata ujuzi wa kujenga kitalu nyumba pamoja na kulima bustani kwa kutumia teknolojia, hiyo ili kuongeza tija katika kilimo na kuvutia vijana wengi kujiajiri kupitia kilimo.
“Tumejipanga kuhakikisha wale wote wanaojihusisha katika sekta hii ya kilimo tuwasaidie watoke hapa waende mbele zaidi sababu aina maana kama serikali tukitumia fedha nyingi za walipa kodi kuwekeza hapa alafu hakuna muendelezo malengo na matarajio yetu ni kuwaunganisha vijana hawa na taasisi za serikali ikiwemo sido ili pia nao washiriki katika uchumi wa viwanda” amesema.
Aidha amesema katika kulitekeleza hilo tayari Serikali imeshatafuta makampuni zaidi ya mawili ambayo yameshaanza kazi ya kutafuta masoko ya bidhaa hizo ndani na nje ya nchi ambayo yataunganishwa na vijana katika maeneo yao ili fedha ambayo inapatikana katika mauzo hayo iweze kuzunguka na kuwasaidia vijana wengine .