Mwandishi wetu- Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema wizara kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), itaendelea kuwaondoa wadaiwa sugu wa kodi ya pango za majengo na nyumba ambao ni watumishi wa umma, wabunge na baadhi ya Taasisi za Serikali.
Alisema lengo ni kuimarisha wakala huo ili uweze kujiendesha na kukamilisha miradi mingine inayoitekeleza.
Kamwele alisema hayo katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyetaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo.
“Wizara imeamua kufanya hivi kwa mujibu wa sheria kwani wakala unadai wateja wake zaidi ya Sh bilioni 20, tukiendelea kulimbikiza madeni haya, wakala utashindwa kujiendesha na hatimaye kufa kabisa,” alisema Kamwelwe.
Aidha alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 wakala huo umekusanya zaidi ya Sh bilioni 19 kutoka vyanzo vyake vya ndani vya mapato na unatarajia kukusanya zaidi ya Sh bilioni 114 katika mwaka wa fedha 2019/20.
Alisema hadi kufikia Juni, 2019 TBA imekamilisha baadhi ya miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba kwenye mradi wa kufufua umeme Rufiji mkoani Pwani.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, akiwasilisha taarifa ya sekta hiyo, aliielezea kamati hiyo kuwa Serikali inaendelea kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege hapa nchini na tayari Sh bilioni 5.7 zimepokelewa wizarani kwa ajili ya fidia ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso, aliishauri wizara kupitia wakala huo kuhakikisha inaondoa kero na malalamiko ya wateja wake kwa kufanya maboresho ya nyumba zake.
Aliishauri Serikali iangalie namna ya kuwapatia wakala mfuko wa dharura kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyosimama hususani ile ambayo ipo katika hatua ya kuiongezea Serikali gharama kubwa kwa kutoendelea kwa ujenzi huo.