32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Petit Afro atoa siri ya ‘Afro Dance’ kupendwa Ulaya

*Beyonce amposti, amgusia mtoto Angel

CHRISTOPHER MSEKENA

KUTANA na Petit Afro, Mtanzania ambaye ni dansa wa Kimataifa na mwalimu wa Afro Dance anayeishi Amsterdam nchini Uholanzi, aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kufundisha na kucheza nyimbo zenye mahadhi ya Kiafrika.

Mapema wiki hii, Swaggaz lilipata nafasi ya kupiga stori ya Petit Afro, kuhusu mambo kadha wa kadha ya sanaa yake na kuipaisha zaidi Afro Dance kwa ujumla. Karibu.

SWAGGAZ: Nafahamu ulikuwa mpiga picha, ilikuwaje ukaingia kwenye uchezaji muziki?

Petit Afro: Unajua kila mtu ni lazima ufanye kitu ukimaliza shule, huwezi kukaa tu nyumbani, lakini mimi mpira siwezi kucheza ikabidi niwe mpiga picha, nimepiga sana picha, mwaka 2012 kuna siku nilikuwa klabu napiga picha kukawa na mashindano ya kucheza Azonto.

Nikacheza nikashinda, kuna mwalimu mmoja ana shule ya dansi akaniambia ameniona nimecheza vizuri ‘African Dance’, njoo ufundishe shuleni kwangu, basi nikaanza kufundisha watoto, wakapenda na kuthamani ninachofanya, nikawa nafundisha hapo shuleni na nje pia nikajiongeza nikawa na darasa langu, ndiyo hivyo nikawa Petit Afro.

SWAGGAZ: Kwanini uliamua kuwafundisha zaidi watoto?

Petit Afro: Hiyo ilitokea kwamba watoto wengi kwenye shule niliyokuwa nafundisha kulikuwa na wanafunzi wengi watoto, wakatokea kunipenda, nataniana nao sana. Kama unavyojua watu wazima huku Ulaya kila mtu yupo bize, anaweza kuja darasani leo, wiki ijayo haji kwahiyo unashindwa kuendelea kufundisha, kila siku unaanza upya ndiyo maana nikaona niwafundishe watoto sababu wana muda, wanapenda na hawafikirii kushindwa, wanapambana kwa nafasi zao, wanacheza wanafurahi wanarudi nyumbani.

Pia nawasaidia watoto hawakai mtaani, nawatoa mtaani harafu kwa watoto ambao hawajiwezi, serikali huwa inawalipia. Kila mtoto lazima awe na kitu cha kufanya, huwezi kukuta mtoto ametoka shule hana cha kufanya labla awe hataki yeye mwenyewe.

SWAGGAZ: Wepesi wa kushika mafunzo ya kucheza kwa watoto upoje?

Petit Afro: Uelewa wao upo kama shuleni tu una tofautiana, kuna mwingine anaelewa ndani ya wiki moja, maana huwa nafundisha mara moja kwa wiki, lisaa limoja mpaka masaa manne, kuna mwingine ndani ya lisaa limoja anaicheza ile dansi kama ameitunga yeye, kuna mwingine mpaka ajifunze mara mbili, kuna mwingine mpaka mara nne, kuna mwingine mpaka nimtumie video nyumbani afanye kama ‘home work’ kwahiyo uelewa wao ni tofauti.

SWAGGAZ: Kwa upande wa mtoto Angel  ilikuwaje?

Petit Afro: Yule Angel nilikutana naye akiwa na miaka sita au saba hivi, alikuwa mdogo sana. Katika lile darasa tulikuwa tunafundisha watoto kuanzia miaka nane na kwendelea, nikaulizwa huyu Angel miaka saba vipi?, nikasema ngoja nimuangalie, niliingia ndani nikaweka muziki nikamwona anavyo ‘move’, akitingisha kichwa namwona kabisa ananata kwenye biti.

Nikasema ngoja nimwangalie kama mwezi hivi, nikamwambia mwenye shule kwamba anaweza, wakaniuliza una uhakika, nikasema ndiyo. Baadaye kwenye darasa la kina Angel lilikuwa na watoto ambao ndiyo wanaanza, nikamwambia yule mwenye shule Angel nataka nimuweke kwenye dasara linalofuata la watoto wa miaka 14-15, akasema hiyo haiwezekani labla kama utaichukua kama ‘riski’ nikasema sawa.

Sababu  nimefanya kazi na watoto kwa miaka mingi, nakuwa najua kabisa uwezo wake, nikawa nawafundisha wale wengine wakubwa wakishaweza, narudi kwa Angel naanza kumfundisha pole pole, wale wengine wakawa hawapendi, alipofika miaka nane, Angel akawa tayari, nikafanya naye video ambayo hiyo ilisambaa siyo mchezo sasa hivi YouTube imetazamwa na watu milioni 32, ilipiga milioni 2 ndani ya mwezi, harafu tena tukacheza wimbo Rockonolo ile ya Diamond, nayo kwa Tanzania ikafanya vizuri zaidi, nikamwambia yule mwenye shule na mama Angel kuwa niliwaambia, Angel akawa staa wa wale watoto wengine wote.

Kwa hiyo ndiyo hivyo ninavyofanya, naanza kufundisha watoto mpaka wakitimiza miaka 17 hivi nawaachia, narudi tena chini kufundisha watoto wengine. Nimefanya ivyo kiasi kwamba kuna wanafunzi wangu wengine ni walimu wanafundisha Afro Dance hiyo inanisaidia hata siku nikifungua shule yangu hao ndiyo watakuwa walimu, kama vile ulivyo mfumo wa mpira wa Barcelona.

SWAGGAZ: Kwanini umeamua kutumia zaidi mtindo wa Kiafrika katika mafunzo yako ya kucheza?

Petit Afro: Wanakwambia wape watu kitu ambacho hawana, Ulaya kulikuwa na Hip hop, Break-dance,  Popping, Afro Dance haikuwepo na ndiyo maana wameipenda sababu ni kitu kipya wenyewe wanasema Afro Dance ni staili fulani ipo ‘happy happy’, watoto muda mwingine huwa wanakataa kutoka na familia zao kwenye sikukuu mbalimbali mpaka waje kwanza kwangu wacheze ndiyo warudi kusheherekea na familia zao.

SWAGGAZ: Hivi karibuni Beyonce aliweka video yako kwenye Instagram (Insta Story) yake ukicheza wimbo wake Don’t Jealous Me, uliipokeaje hiyo?

Petit Afro: Nilipokuwa nafanya ile video hilo ndiyo lilikuwa lengo ingawa lengo langu haswa lilikuwa kwa mama yake Beyonce, mama yake ndiyo aliiweka kabisa kwenye ukurasa wa Instagram, unajua ni ngumu Beyonce kukuposti kwahiyo nilifurahi.

SWAGGAZ: Malengo yako zaidi ni yapi kwenye Afro Dance?

Petit  Afro: Malengo yangu yalikuwa niwe wa Kimataifa, sasa nimeshakuwa ‘International’, nilichofanya Ulaya kama nilivyokwambia mimi siyo yule mwalimu ambaye nafundisha harafu naondoka.

Mimi ndiyo huwa nawafungulia watoto akaunti zao za Instagram, siyo mama zao, ndiyo maana majina yao utaona  @angel.afrodance, @nyah.afrodance, @leyla.afro ni kama cheni fulani hivi ya Afro kwa maana kwamba wale watoto wakiwa maarufu wataweza kupata chaneli zao.

Kama unavyoona sasa hivi mtoto Angel anafanya mitindo, yupo kwenye matangazo mbalimbali na wanaitwa kwenye video mbalimbali, wanatumbuiza kwenye ‘birthday party’ za watoto wenzao, kwahiyo ndiyo hivyo wananufaika.

Nikasema kama nimefanya hivyo hapa Ulaya watu wanapenda na Ulaya watu walianza kupenda dansi baada ya TV mbalimbali kuleta mashindano ya kucheza na watu wanashinda fedha nyingi, lakini Tanzania sioni, ndiyo maana nimekuja Tanzania niangalie mipango inaanzia wapi, sheria zinasemaje, vipaji vyenyewe navipatia wapi, najua wapo ila hawapo mitandaoni kama nchi zingine.

Ndiyo maana juzi nimeenda Afrika Kusini huko Cape Town na Johannesburg, nimeshapata watoto na nina watoto wengine Uganda wengine wapo Nigeria na lengo langu ni kwa watoto na vijana ila changamoto ndiyo hivyo wazazi ni watata, watoto hawana shida sana sana wanawake.

SWAGGA: Hongera pia kwa kufikisha wafuasi (subscribers) milioni moja YouTube.

Petit Afro: Nashukuru, wale wote wametoka nchi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles